
MWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambaye pia ni mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Rais Dkt. John Pombe Magufuli amewaasa wananchi wa Zanzibar kumchagua Dkt. Hussein Ali Hassan Mwinyi kuwa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar badala ya kuchagua mgombea wa chama pinzani ambaye bila kumtaja kwa jina, rais Magufuli amesema ni mzee na amekuwa akigombea kila mara na anashindwa.
Magufuli amesema hayo leo Jumamosi,. Julai 11, 2020 wakati akihutubia mara baada ya kuchaguliwa kwa kishindo cha kura 1,822 (asilimia 100) kuwa mgombea urais wa Tanzania kupitia CCM na Dkt. Mwinyi kupitishwa na chama hicho kuwania urais wa Zanzibar.
“Wewe ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ukifika kule Zanzibar unaanza shikamoo mheshimiwa, inachosha. Msinichagulie shikamoo huko Zanzibar nitapata shida ndugu zangu. Na mimi nataka nikija Zanzibar nije kwa raha zote. Nani Sultani? Anayegombea kila mwaka au anayegombea mara moja akashinda?
“Hussein Mwinyi namzidi umri, kanichagulieni huyu na mimi nitajisikia raha, sio mkanichagulie Mtu ambaye nikifika Zanzibar nitamuambia Shikamoo, inachosha, msinichagulie shikamoo mtanipa tabu, nichagulieni huyu nitampa nguvu zote kwakuwa ni Mdogo wangu.
Hussein Mwinyi ni mnyenyekevu sana, hajaubeba Urais wa Baba yake, na ndio maana wakati anashukuru hapa hajaanza kumshukuru Baba yake, kamshukuru Mkapa, akamshukuru Kikwete kisha kanishukuru mimi akafuata Baba yake, Mwinyi ana hekima.
“Nawaambia hii siri, Hussein Mwinyi nilimteua kuwa Mgombea Mwenza pamoja na Mama Samia, lakini kwakuwa Mama Samia ni Mwanamke akashinda kuwa Makamu wa Rais, maana huwezi kushindana na Wanawake ukashinda, Wanawake wanatuzidi kwa mambo mengi, Wanawake oyee”
“Kama atachaguliwa Mwinyi, tutayaona Matokeo, maomba Wazanzibari achaneni na Upemba na Uunguja, Ukaskazini wala Ukusini na muwe na Zanzibar yenye maendeleo.
“Nitoe wito kwa Vyama vya siasa tusiwe na Wagombea haohao, tubadilishe Sample, sio kila siku Watu walewale, Mungu hajakuumba wewe tu kwamba uwe Kiongozi kila siku, tuwaachie wengine, Mzee Kikwete angeweza kuendelea kuwa Mwenyekiti ila aliniachia na waliotangulia hivyohivyo,” amesema Magufuli.