
LEBO ya muziki ya Wasafi Classic Baby (WCB) inayomilikiwa na msanii Diamond Platnumz imetangaza kufanya shoo ya kuwashukuru Watanzania na wadau wote wa muziki pamoja na vyombo vya habari kwa mapokezi mazuri kwa msanii wao mpya, Zuhura Kopa, maarufu kama Zuchu. Shoo hiyo itafanyika usiku wa Julai 18, 2020, katika Ukumbi wa Mlimani City, jijini Dar es Salaam.
Hayo ameyasema leo Jumatatu, Julai 13, 2020 wakati akizungumza na wanahabari katika Ukumbi wa Mikutano wa Hoteli ya Hyatt Regency jijini Dar es Salaam.
Alichokisema Zuchu baada ya kutambulishwa:
“Kukiwa na wanawake wawili sehemu moja maneno lazima yatengenezwe, mimi na Queen Darleen hatuna tatizo na hata ikitokea siku akanikosea sitomvunjia heshima. Kuna siku alinikuta njiani nalia akanibeba kwenye gari nikaenda kulala kwake, ananitia moyo sana.
“Kumsimamia msanii wa kike ni kazi ngumu sana lakini nashukuru menejimenti yangu ya WCB wamefanya kazi kubwa kunifikisha hapa nilipo. Shoo ya Julai 18, 2020, itakuwa ni nafasi ya muhimu kufanya shoo yangu ya kwanza kubwa tangu niingie rasmi kwenye muziki.
“Nataka kuwagusa wanawake wenzangu, najua kwenye shoo yangu ya Julai 18, 2020, asilimia 30 ya mapato yatakayopatikana yatakwenda kumsaidia mwanamke yeyote mwenye uhitaji maalum popote alipo.
“Vaa pendeza, njoo Mlimani City, siku hiyo itakuwa ni ya kufurahi zaidi. Wasanii wote wa kike tiketi zenu nimewaandalia zitakuwepo, natamani siku hiyo mama yangu (Khadija Kopa) awepo, natamani dada yangu, Lady Jaydee, anielekeze vitu vichache vya kufanya kwenye shoo,” amesema Zuchu.