
MWANAMITINDO na mjasiriamali, Flaviana Matata amezindua bidhaa zake mpya za taulo za kike (pedi) alizozipa jina la ‘Lavy Sanitary Pads’ huku lengo kuu likiwa ni kusaidia wanafunzi hasa wasichana wasiokuwa na uwezo.
Akizungumza na Global Publishers leo katika ukumbi wa Hyatt Regency jijini Dar Es Salaam, mrembo huyo mwenye mvuto wa aina yake alisema kwamba lengo la kuanzisha bidhaa hizo ni kutaka kusaidia watoto wa kike ambao hawana uwezo wa kununua pedi pindi wanapopata hedhi hali inayosababisha kukosa masomo.
Aidha aliendelea kueleza kwamba taulo hizo zina ubora, usalama wa hali ya juu na bei rafiki. Bidhaa hii imeambatana na kauli mbiu ya ‘SIKU ZAKO NI SIKU ZETU’ yenye lengo la kuvunja ukimya na kuondoa dhana hasi kwenye suala la hedhi katika jamii.
“Hii imekuwa ni ndoto yangu niliyokuwa naifanyia kazi kwa miaka sita (6) sasa, lengo kubwa ni kuhakikisha mtoto wa kike hakosi kuhudhuria masomo yake au kufanya shughuli nyingine ya kimaendeleo kutokana na changamoto za hedhi.
“Pia kuondoa dhana kwa mtoto wa kike na jamii kwa ujumla kuwa hedhi ni kitu cha aibu, siri na cha uchafu kama inavyochukuliwa na baadhi ya watu,” alisema Flaviana Matata.
Stori: Memorise Richard na Happyness Masunga