
WASHINDANI wawili kunako Bongo Fleva, Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’ na Ali Saleh Kiba ‘King Kiba’, wameacha gumzo jijini Dodoma walipohudhuria Mkutano Mkuu wa Taifa wa CCM.
Diamond au Mondi ambaye ni C.E.O wa Lebo ya Wasafi Classic Baby (WCB), alifuatana na wasanii wake ambao ni Abdul Idd ‘Lava Lava’, Yusuph Mbwana ‘Mbosso’, Zuhura Kopa ‘Zuchu’, Raymond Mwakyusa ‘Rayvanny’ na Mwanahawa Abdul ‘Queen Darleen’.
Kwa upande wa Zuchu alipanda jukwaani na kupafomu huku akisindikizwa na wasanii wengine kutokea lebo hiyo.
Mbali na timu ya wanamuziki wa Wasafi pia mameneja wa lebo hiyo, Hamis Taletale ‘Babu Tale’ na Said Fela ‘Mkubwa Fela’, nao walihudhuria mkutano huo.
Naye C.E.O wa Lebo ya King’s Music Records, King Kiba alitinga jijini Dodoma akiwa na timu yake na alipanda jukwaani akaangusha bonge moja ‘pafomansi’.
Mbali na wanamuziki hao wakubwa na timu zao, pia wasanii wengine waliopanda jukwaani na kutoa burudani kwenye mkutano huo ni pamoja na Abdul Chande ‘Dogo Janja’, Hamis Mwinjuma ‘MwanaFA’, William Lymo ‘Billnass’ na Nurdin Bilal ‘Sheta’.
Wengine ni Omari Mwanga ‘Marioo’, Hamad Ally ‘Madee’ Haidari Said ‘Bob Haisa’ Hamza Kalala na wengine wengi.
Wasanii wa filamu waliohudhuria mkutano huo ni pamoja na Halima Yahya ‘Davina’, Steven Mengere ‘Steve Nyerere’ na wengine, lakini gumzo kubwa likabaki kwa Mondi na Kiba kwani kwa muda mrefu hawakutana uso kwa uso.
Mkutano huo Mkuu wa CCM Taifa 2020 umefanyika kwenye Ukumbi wa Jakaya Kikwete ambapo umehudhuriwa na viongozi wa zamani wa nchi kama Rais wa Awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi, Rais wa Awamu ya Tatu, Benjamin William Mkapa na Rais wa Awamu ya Nne, Dk Jakaya Mrisho Kikwete.
STORI: HAPPYNESS MASUNGA, DAR