×

JB Amwaga Mil 400 Kwenye Tamthilia!

MUITE DJ Benny, Bonge la Bwana, Eric Ford na mengine mengi. Huyu ni muigizaji mkubwa na wa kitambo kunako Bongo Movies.

Jina lake halisi ni Jacob Steven almaarufu JB. Amewahi kutamba na michezo ya kuigiza enzi hizo za Mambo Hayo na anatamba na sinema zenye majina makubwa kama Mahabuba, Shikamoo Mzee, Mzee wa Swaga, Senior Bachelor, 14 Days, Chungu cha Tatu, DJ Ben, Danijo na nyingine lukuki.

Mbali na filamu, amefanya na anafanya vizuri kunako tamthiliya mbalimbali kama Kisasi, Slay Queen na nyingine.

Wakati baadhi ya waigizaji wakidai soko la sinema sasa hivi limeyumba, hivyo hata sinema zenyewe haziuzi ndiyo maana wamepumzika kwa muda, hii imekuwa ni tofauti kwa JB kwani anasema anatengeneza pesa nyingi kupitia Bongo Movies.

IJUMAA WIKIENDA limekusogeza karibu na JB kwenye mahojiano maalum (exclusive) ambapo anafunguka mengi kuhusiana na kazi yake ya sanaa na ujio wa tamthiliya yake mpya. Ungana naye hapa chini.

IJUMAA WIKIENDA: Umekuja na Tamthiliya ya Single Mama, je, mashabiki watarajie nini?

JB: Mashabiki wanatakiwa wajue kuwa nimeamua kuja na Single Mama kwa sababu katika kila wanawake kumi wenye watoto, wanawake watano wanalea peke yao. Kwa hiyo, hili ni tatizo kubwa, lakini halionekani, ni tatizo la Dunia siyo Tanzania au la Afrika tu, wanawake wanaolea watoto wenyewe ni wengi.

IJUMAA WIKIENDA: Je, tamthiliya hii ina ‘seasons’ ngapi na itaanza kuruka lini na sehemu gani?

JB: Tamthiliya itakuwa na seasons 10 ambazo kila season itakuwa na episode 20, jumla tunatengeneza episode 200. Katika episode 20 za kwanza, tunaonesha ilikuwaje hadi wakazalishwa ‘masingo mamaz’ ili watu wavae viatu vyao na tujue kama tunaweza tukawalaumu.

IJUMAA WIKIENDA: Nini lengo la kuja na Tamthiliya ya Single Mama?

JB: Tunachotaka mke na mume wakiwa wanaangalia hii tamthiliya, waanze kujikosoa kama kuna tatizo na kama kuna ambao tayari hawapo pamoja ila wamejaaliwa kuzaa na kutokana na matatizo yao wanaona hawataweza kurudiana, basi wakubaliane kulea mtoto.

IJUMAA WIKIENDA: Kumekuwa na ushindani mkubwa kwenye tamthiliya, wakati wewe unatarajia kuanza kuonesha ya kwako, lakini tunaona Ray, Single Mtambalike na wengine, nao wana tamthiliya zao, vipi kwa upande wako umejipangaje?

JB: Nipo kwenye fani hii kwa zaidi ya miaka 20, ninachotafuta sasa ni heshima.

IJUMAA WIKIENDA: Katika sinema zako, ni ipi unaikubali zaidi?

JB: Hakuna sinema iliyowahi kunipa heshima kama 14 Days. Kwenye 14 Days tulizungumza kitu kama hiki, kuna kapo ilikuwa inasumbuana, lakini tukazungumza namna nzuri ya kutibu tatizo.

IJUMAA WIKIENDA: Na ilikupa mafanikio kiasi gani?

JB: Tulipata mialiko mingi ndani na nje ya nchi, watu wengi walioitazama ilikuwa kama dawa kwao, kwa maana hiyo basi, mbali na kwamba tunafanya ushindani, lakini pia tunatengeneza suluhisho.

IJUMAA WIKIENDA: Kuna akina singo mamaz wengi na kila mmoja ana sababu iliyomfanya awe hivyo, je, kwa upande wako umelenga kuzungumzia singo mamaz wa aina gani?

JB: Kwa vyovyote vile, hii tamthiliya itagusa maisha ya kila mtu, hapa tunazungumzia singo mamaz wa aina tano, kuna wa kipato cha chini, kati, wa juu kidogo, matajiri na wale wanaokaa kwao.

IJUMAA WIKIENDA: Ni kitu gani cha tofauti ulichokifanya kutokana na uzoefu wako?

JB: Mada tuliyoichagua ni ya tofauti na tumetoa elimu, waigizaji tuliowatumia ni bora na tumewaona kwenye sekta ya sanaa na vyuoni.

IJUMAA WIKIENDA: Tamthiliya hii inagharimu kiasi gani?

JB: Bajeti ya Single Mama ni shilingi milioni 400.

IJUMAA WIKIENDA: Kampuni yako ya Jerusalemu Films imeachana na sinema na kubaki na tamthiliya tu?

JB: Bado tunatengeneza sinema, ila kwa sasa tunatengeneza tamthiliya.

IJUMAA WIKIENDA: Waigizaji wengi wamekuwa wakitumia ‘application’ katika kutangaza kazi zao, je, kwa upande wako imekaaje?

JB: Hatuwezi kushindana na teknolojia, hivyo tutafanya jinsi inavyotupeleka, tulianza kuigiza na mikanda, ila kwa sasa hakuna.

IJUMAA WIKIENDA: Umekuwa kwenye tasnia kwa muda mrefu, je, unaionaje kimataifa?

JB: Niko tofauti na wengine, ninachokifahamu kufanya kazi kimataifa, ni kufanya popote ulipo ila kazi yako ikidhi kiwango cha kimataifa. Sina maana kwamba sipendi, ila tunatakiwa kuitengeneza tasnia ili watu wengine watamani kuja kuigiza na hii itatoa fursa ya kuongeza kipato.

IJUMAA WIKIENDA: Je, Bongo Movies inakidhi viwango?

JB: Ndiyo, naona inakidhi viwango vya kimataifa.

IJUMAA WIKIENDA: Umekuwa ni muigizaji ambaye uko mbali na skendo, je, unaepuka vipi?

JB: Maisha ni kuamua.

IJUMAA WIKIENDA: Unapitia changamoto gani kwenye kazi zako?

JB: Usambazaji ni tatizo kubwa na ndiyo maana kwa sasa tamthiliya zinaibuka kwa sababu hakuna msambazaji mzuri wa sinema.

IJUMAA WIKIENDA: Kuna kipindi ulikuwa ukipunguza mwili, je, bado unaendelea?

JB: Watanzania wanatakiwa wajue sina shida na mwili wangu.

IJUMAA WIKIENDA: Ulishawahi kupata dili lolote kutokana na mwili wako?

JB: Nimefanya matangazo mengi na nimekuwa balozi wa vitu vingi.

IJUMAA WIKIENDA: Ni muigizaji gani wa kike unamkubali zaidi?

JB: Mimi ni kama baba, niko karibu na waigizaji wote.

IJUMAA WIKIENDA: Umekuwa shabiki mkubwa wa mpira, unazungumziaje ligi za ndani na nje ya Tanzania?

JB: Mimi naweza kusema, Simba wamejipanga, ndiyo machampioni na kwa upande wa nje Liverpool ni championi siku zote, umri ungekuwa unaruhusu, ningeichezea Simba na Liverpool.

IJUMAA WIKIENDA: Kwa upande wako imekaaje nia ya kutangaza kugombea ubunge kama walivyofanya wengine?

JB: Sifikirii kazi nyingine yoyote zaidi ya sinema.

IJUMAA WIKIENDA: Sanaa imekupa mafanikio gani?

JB: Sinema zimenipa pesa nyingi mno hadi naogopa.

IJUMAA WIKIENDA: Una shilingi ngapi benki?

JB: Wewe jua tu nina pesa.

MAKALA: MEMORISE RICHARD NA HAPPYNESS MASUNGA, BONGO

Leave a Comment