×

Maisha Mapya ya Kiba, Mondi!

 

DAR: Yaliyopita si ndwele, tugange yajayo! Ndivyo unavyoweza kusema kufuatia mastaa wawili ndani ya Bongo Fleva; Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’ na Ali Saleh Kiba ‘King Kiba’ kufungua ukurasa mpya wa maisha, IJUMAA linakupa mchapo kamili.

 

Maisha mapya ya mastaa hao yanakuja baada ya hivi karibuni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk John Pombe Magufuli ‘JPM’ kuwakalisha meza moja kwenye hafla ya chakula cha mchana kwa wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) huko Ikulu- Chamwino jijini Dodoma.

 

Chanzo makini kimelieleza Gazeti la IJUMAA kuwa, mara baada ya kupatanishwa, wawili hao kwa sasa hawatakuwa wakiishi kwa uadui kama mwanzo, bali watashindana kimuziki tu.

 

“Ule uadui wa kutokusalimiana, kutozungumziana mambo mazuri kwenye vyombo vya habari, ndivyo vilizikwa pale Dodoma, lakini kuhusu muziki, maisha yao mapya sasa hivi yatakuwa mazuri.

 

“Watakuwa wanapeana ushauri wa kimuziki, watakuwa wanapeana michongo na mambo mengine ambayo zamani ilikuwa ni vigumu. Lakini hii haimaanishi kwamba hawatakuwa na ushindani wa kimuziki, huu utaendelea kuwepo. Watakuwa wanashindana kama kawaida ili kuleta chachu kwa mashabiki,” kilisema chanzo na kuongeza;

 

“Huwenda pia wakafanya kolabo ya pamoja, kwani itakuwa ni ishara tosha ya kuwaaminisha mashabiki wao kwamba hakuna mwenye kinyongo na mwenzake.”

 

MONDI AZUNGUMZA

Gazeti hili la IJUMAA lilifanikiwa kufanya mahojiano na Mondi hivi karibuni ambapo pamoja na mambo mengine, alisema wameshayamaliza na yeye hana kinyongo chochote.

 

“Unajua siku zote mitandao ndiyo huwa inatugombanisha, lakini binafsi sina tatizo na kaka yangu, Kiba ni mtu ambaye alinitangulia kwenye muziki na bado anafanya vizuri, pia Harmonize (Rajab Abdul) ni kijana mwenzangu ambaye tulikutana na kusaidiana kwenye muziki na nafurahi kuona bado anapambana, hivyo kitendo alichokifanya Rais kutukalisha meza moja, ilikuwa ni jambo jema,” alisema Mondi.

 

MENEJA WA MONDI AFUNGUKA

Pia Gazeti la IJUMAA lilifanikiwa kuzungumza na meneja wa Mondi, Said Fela ‘Mkubwa Fela’ ambapo kwa upande wake alisema kitendo alichokifanya Rais Magufuli ni kikubwa na atakikumbuka mpaka anaingia kaburini.

 

“Kwanza tunamshukuru Rais kwa sababu Rais ndiyo baba yako wa dunia, wa nchi yako na kiongozi wako, kwa hiyo alichokifanya kumkalisha Nasibu na wasanii wenzake ni kitu kikubwa, binafsi nitakiweka kwenye moyo wangu kama kumbukumbu mpaka nakufa.

 

“Kwa sababu mwisho wa siku hatunaga tofauti zile za kwenye mioyo, ila tofauti zinajengwa na media, watu binafsi wenye maslahi na hayo matatizo, kwa hiyo sisi tunashukuru Rais kutuunganisha kuwa wote wamoja, lakini sisi wengine tunapenda tushindane kwenye kazi, ila tusishindane kwenye utaifa wetu,” alisema Fela.

 

VIPI KUHUSU KOLABO?

Gazeti la IJUMAA lilimuuliza meneja huyo kama wana mpango wa kufanya kolabo na Kiba pamoja na Harmonize baada ya kuwa sasa mambo yao yapo safi, lakini alijibu kwa kifupi tu kuwa hawezi kuzungumza.

 

“Kwa sasa hivi nikisema niongelee kuhusu kolabo nitakuongopea, mimi naona tuishie hapa tu,” alisema Fela.

Stori: Memorise Richard na Happynes Masunga, Ijumaa

Leave a Comment