×

Siri Mastaa Kujitosa Ubunge Yafichuka!

DAR: Wakati mbio za Uchaguzi Mkuu mwaka huu zikizidi kushika kasi, nafasi ya ubunge imetia fora kwa kuvutia mastaa wengi na watu wa kada mbalimbali, hali inayosababisha baadhi ya Watanzania kujiuliza nini kimewaibua watia nia hao sasa, Gazeti la IJUMAA linaripoti.

Licha ya kwamba Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ibara ya 67 (1) inawaruhusu mastaa hao kuwania nafasi hizo, wingi wao kwenye uchaguzi wa mwaka huu, umebainika kuchangiwa na siri tano nyumba ya pazia zilizowahamasisha kujitosa kwenye kuwania nafasi ya ubunge.

Baadhi ya mastaa waliojitosa ni pamoja na wasanii wa filamu, muziki wa Bongo Fleva, watangazaji maarufu na wadau wengine wanaogusa tasnia ya sanaa nchini.

MAFANIKIO YA WABUNGE WASANII

Mojawapo ya siri walioitaja watia nia hao kupitia vyama mbalimbali vya siasa nchini, ni mafanikio ya wasanii walionyakua ubunge katika uchaguzi mkuu wa 2015.

Baadhi ya wasanii wabunge waliotajwa ni Joseph Mbilinyi ‘Sugu’, Joseph Haule ‘Profesa Jay’ na Vicky Kamata.

Mastaa hao walisema kuwa, ushiriki wa wabunge hao katika siasa za Tanzania kuanzia 2015 hadi sasa, umewaondolea hofu ya kujitosa kuwania ubunge.

Mr Two au Sugu kama wengi wanavyomuita, alikuwa Mbunge wa Mbeya-Mjini kupitia tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), anatajwa kuwa na mijengo ya kifahari Dar na Mbeya. Pia anamiliki hoteli ya kitalii yenye hadhi ya nyota tatu jijini Mbeya mbali na magari ambayo pia yametajwa kuwavutia mastaa kujitosa katika ubunge mwaka huu.

Aidha, harakati za Profesa Jay ambaye alikuwa Mbunge wa Jimbo la Mikumi (Chadema), nazo zimedaiwa kuwavutia mastaa hao kutokana na nyimbo kali alizokuwa anazitoa kuhusiana na siasa.

Profesa Jay ni miongoni mwa wasanii wakubwa walioupaisha muziki wa Bongo Fleva na kumfanya aliyewahi kuwa Waziri Mkuu, Joseph Warioba kumsifia alipotoa Ngoma ya Ndiyo Mzee iliyopiga ‘madongo’ kwa wanasiasa.

Vivyo hivyo ndivyo ilivyokuwa kwa upande wa Mbunge wa Viti Maalum (CCM), Vicky Kamata ambaye pia alijizolea umaarufu kwa wimbo wake wa Wanawake na Maendeleo.

Historia ya msanii huyo na mafanikio aliyonayo sasa, pia imeelezwa kuwa ni mojawapo ya sababu zilizowavuta mastaa wengi kutosha katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu.

ANGUKO LA SANAA

Baadhi ya mastaa waliojitokeza mwaka huu kutaka kuwania ubunge, ni wasanii ambao tayari walikuwa ‘wamechuja’, wamepoteza umaarufu kutokana na kudorora kwa fani ya sanaa nchini hususan filamu kasha baadhi wa Bongo Fleva.

Anguko hilo limethibitishwa hivi karibuni na Msanii wa Bongo Fleva; Vanessa Mdee ambaye alitangaza kuacha muziki kwa kuwa hauna faida na kuongeza kuwa amechoka kuishi maisha ya kuigiza.

Kutokana na hali hiyo, baadhi ya wachambuzi wa sanaa, wameeleza wazi kuwa, utitiri wa wasanii hao kujitosa kuwania ubunge, ni njia mojawapo ya kujikwamua kimaisha.

Ikumbukwe kuwa, inaelezwa kuwa mshahara wa mbunge ni zaidi ya shilingi milioni 12 kwa mwezi, ilihali akipokea kiinua mgongo cha shilingi milioni 240 baada ya kumaliza ngwe yake ya miaka mitano.

UBUNGE SASA ‘NJIA NYEUPE’

Aidha, imeelezwa kuwa, utitiri wa wasanii hao kuwania ubunge, pia imetokana na hamasa inayotolewa na Mwenyekiti wa CCM, Rais John Magufuli pamoja na viongozi wengine katika kudhibiti matumizi makubwa ya pesa kwenye chaguzi.

Hali hiyo ilikuwa inawapa hofu vijana kujitokeza kuwania ubunge wakiwamo mastaa, lakini sasa hali imekuwa tofauti baada ya vitendo vya rushwa kudhibitiwa.

Hata hivyo, mtazamo wa majukumu ya mbunge, yameonekana kutokuwa na ugumu kwa Watanzania kujitokeza kuwania nafasi hiyo wakiwamo mastaa.

MAGUFULI AMEWAVUTA

Mbali na kudhibiti vitendo vya rushwa, baadhi ya wachambuzi wamelieleza Gazeti la IJUMAA kuwa, kasi ya utendaji na usimamizi wa majukumu katika Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Magufuli, ni mojawapo ya mambo yaliyowavutia Watanzania wengi wakiwamo mastaa kuwania ubunge.

Kasi yake ya utekelezaji wa ahadi kama vile ujenzi wa reli ya kisasa, ujenzi wa miundombinu, ununuzi wa ndege, kuwatengenezea mazingira mazuri wafanyabiashara wadogo ‘wamachinga’ pamoja na kuboresha huduma za kijamii, pia imeelezwa kuwavutia Watanzania kutaka kushiriki siasa ili kuijenga nchi yao zaidi.

KUJIFUNGAMANISHA NA DOLA

Aidha, wachambuzi wamefafanua kuwa mastaa wengi wanaitazama nafasi hiyo ya kutia nia kama mojawapo ya lengo la kujipitisha na kuonekana kwa wakuu ili kupata bahati ya teuzi katika siku za usoni iwapo wakiukosa ubunge.

Hali hiyo imedhihirika zaidi kwa mastaa waliojitokeza kuchukua fomu kuwania kuteuliwa kuwa mgombea ubunge kupitia CCM kwa sababu ni chama tawala kinachoaminika kuendelea kushika dola baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka huu.

“Kwa sababu ndani ya CCM, kada anapokosa kuteuliwa kuwa mbunge au nafasi nyingine, yamkini anaweza kuja kuteuliwa kuwa mkuu wa mkoa, mkuu wa wilaya, katibu tawala, mkurugenzi wa halmashauri pamoja na nafasi nyingine kedekede,” alisema msanii wa filamu, Kulwa Kikumba ‘Dude’.

Baadhi ya mastaa waliojitokeza kuwania nafasi ya ubunge kupitia vyama mbalimbali ni pamoja na; mshereheshaji na msanii wa filamu za Kibongo, Mahsein Awadh ‘Dk Cheni’ ambaye amechukua fomu kuwania ubunge katika Jimbo la Ilala kupitia CCM.

Wengine ni Khamis Mwinjuma ‘MwanaFA, Mtayarishaji nguli wa muziki wa Bongo Fleva, Joachim Kimario ‘Master J’, msanii wa filamu, Steven Mengere ‘Steve Nyerere’, msanii wa filamu za Kibongo, Halima Yahya ‘Davina’ na watangazaji maarufu Bongo, Zamaradi Mketema, Flora Nitetee, Mboni Masimba na Joyce Kiria.

Wengine ni mmoja wa mameneja wa Wasafi, Hamis Taletale ‘Babu Tale’, wasanii wa Bongo Fleva, Baba Levo na Wakazi. Pia yumo mwigizaji Sister Fey na Mwijaku.

Stori: Mwandishi Maalum, Ijumaa

Leave a Comment