
MAOFISA kutoka katika baadhi ya hospitali jijini Antananarivo, Madagascar, wametahadharisha kuwa huenda maeneo ya kutoa huduma yakaelemewa na wagonjwa kutokana na kuongezeka kwa kasi ya maambukizi ya virusi vya corona.
Moja ya hospitali nchini humo imeeleza kuwa ina uwezo wa kuhudumia wagonjwa 50 na tayari wana wagonjwa 46 hivyo kumebaki nafasi ya wagonjwa wanne tu.
Waziri wa Afya wa Madagascar ameandika barua kwenda kwa wakala wa misaada wakiomba kupatiwa misaada ya vipimo, mashine za kupumulia na vifaa kinga kwa ajili ya watoa huduma ili kusaidia mapambano dhidi ya virusi hivyo.
Mwakilishi wa Shirika la Afya Duniani (WHO) nchini humo ametahadharisha kuwa kwa hali ilivyo hospitali zitakuwa na wagonjwa wengi kabla ya kasi ya maambukizi haijafika kileleni.
Zaidi ya visa 7,500 vya maambukizi ya COVID-19 vimeripotiwa nchini humo ambapo zaidi ya 80% ya visa hivyo vimetokea mwezi uliopita.
Katika hatua nyingine kuhusu hali ya virusi hivyo barani Afrika, Rais wa Liberia, George Weah, ameondoa hali ya hatari iliyotangazwa Aprili 2020 kwa lengo la kupambana na virusi hivyo.