
SERIKALI ya Marekani imeitaka China kufunga ubalozi wake mdogo katika jiji la Texas katika Jimbo la Houston, kufikia Ijumaa — hatua iliyoelezewa kama “uchokozi wa kisiasa” na Beijing.
Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani imesema kuwa uamuzi huo unalenga “kulinda hakilimiliki ya Wamarekani “.
Wizara ya Mambo ya Nje ya China imesema ikilaani vikali uamuzi huo na kutishia kuchukua hatua za kulipiza kisasi. Wakati wa mkutano na waandishi wa habari wa kila siku, msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya China, Wang Wenbin, amesema Beijing iliarifiwa ghafla kuhusu hatua hiyo Jumanne wiki hii.
Hata hivyo, hakutoa sababu za Marekani kuitaka China kufunga ubalozi wake mdogo huko Texas. Mamlaka nchini Marekani imeipa China siku tatu kuwa imefunga ubalozi wake mdogo Texas, Wang Wenbin amesema.
Utawala wa Rais Donald Trump umekuwa na sintofahamu ya mara kwa mara na ule wa Beijing juu ya biashara na janga la virusi vya corona, pamoja na hatua ya China kuweka sheria mpya ya usalama juu ya Hong Kong. Juzi, Jumanne, wizara ya sheria ya Marekani iliishutumu China kwa kudhamini wadukuzi ambao wamekuwa wakilenga maabara zinazotengeneza chanjo za Covid-19.

“Hatua ya Marekani kufunga ubalozi wa China huko Houston, bila hata hivyo kuishirikisha serikali ya Beijing, katika kipindi kifupi kama hiki ni muendelezo wa hatua za hivi karibuni za Marekani dhidi ya China,” Wenbin ameongeza.
“Tunaiomba Marekani kufuta uamuzi huo mbaya mara moja. Kama itaendelea kushikilia uamuzi wake huo mbaya, China italipiza kisasi kwa kuchukuwa hatua kali, ” amebaini msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya China. Msemaji wa wizara ya mambo ya kigeni ya Marekani, Morgan Ortagus, amesema amri hiyo ililenga kulinda hakimiliki za Marekani na taarifa za faragha za raia wa Marekani.
Ubalozi mdogo wa China wa Houston ni moja ya balozi ndogo tano za China zilizopo nchini Marekani, bila kuhesabu Ubalozi wake uliopo Washington DC. Haijawa wazi kuhusu iwapo ubalozi huu pia umetajwa miongoni mwa zile zilizoamrishwa kufungwa.
Bi Ortagus aliongeza kuwa Marekani “haitavumilia ukiukaji wa hadhi ya nchi yetu na vitisho vya Jamuhuri ya Watu wa China (PRC) na kama tu ambavyo hatukuvumilia, utendaji wa biashara usio wa haki wa haki, wizi wa kazi za Wamarekani, na tabia nyingine za uchokozi. “
Bi Ortagus pia alitaja makubaliano ya Vienna kuhusu mahusiano ya kidiplomasia , ambayo yanasema nchi “zina wajibu wa kutoingiliana kuhusu masuala ya ndani” ya nchi mwenyeji.

Katika taarifa tofauti, Wizara ya mambo ya nje ya Marekani iliishutumu China kwa kuhusika “katika ujasusi mkubwa kinyume cha sheria na kushawishi utendaji “, kuingilia “siasa za ndani ” pamoja na “kuwatisha wafanyabiashara wakuu, kuzitisha familia za Wamarekani wanaoishi China, na tuhuma nyingine zaidi “.
China ilitaja uamuzi huo kama uchokozi wa kisiasa, ikisema kuwa unakiuka sheria ya kimataifa. Bwana Wang aliendelea kusema kwamba Washington imekuwa ikiilaumu China kupitia ‘unyanyapaa’ na ‘kuishambulia’ mara kwa mara.
Aliitaka Marekani kufikiria , akisema kuwa iwapo itasisitiza kufuata mkondo huo wa mbaya , ”China italipiza kwa kuchukua hatua kali zaidi.”.