×

Mudathir: Tunataka Heshima Tu Azam FC

KIUNGO wa Azam FC, Mudathir Yahya, amesema licha ya kupoteza nafasi ya kutwaa kombe lolote msimu huu, lakini kikosi chao hakitaacha kupambana kwenye michezo miwili iliyosalia ya Ligi Kuu Bara kwa ajili ya kutunza heshima yao.

 

Azam FC ambayo leo Alhamisi inatarajiwa kupambana na Mbeya City kwenye Uwanja wa Azam Complex, Dar, inaifukuzia nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara ambayo kwa sasa inashikiliwa na Yanga.

 

Mudathir amekiri kuwa, msimu huu haukuwa mzuri kwao, lakini hawajakata tamaa kwa kuwa bado wanaweza kumaliza wakiwa nafasi ya pili licha ya kupata ushindani kutoka kwa Yanga.

 

“Ni kweli msimu huu haujawa mzuri sana kwetu, tulijiwekea malengo ya kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara, lakini kwa bahati mbaya hatujafanikiwa kufikia malengo hayo licha ya kujitahidi kupambana.

 

“Lakini bado tunayo nafasi ya kumaliza msimu tukiwa kwenye nafasi ya pili, hivyo tutajitahidi kuhakikisha tunashinda michezo miwili iliyosalia ili kulinda heshima yetu,” alisema Mudathir.

 

Kabla ya Yanga jana haijacheza dhidi ya Mtibwa, ilikuwa na pointi 68 mbele ya Azam yenye 66. Wikiendi hii Azam itamaliza ligi kwa kucheza dhidi ya Prisons na Yanga dhidi ya Lipuli. Wote watakuwa ugenini.

Leave a Comment