×

Mkapa Ameacha Alama ya Unyenyekevu Kanisani – Padri Casmir Kavishe

 

Makanali wa JWTZ wakiwa wamebeba jeneza lenye mwili wa Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu Marehemu Benjamin William Mkapa wakati wakiingia katika sehemu ya Ibada katika Misa ya Dominika ya 17 ya Mwaka ‘A’ wa Kanisa Katoliki pamoja na Kumuaga Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu Marehemu Benjamin William Mkapa katika Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam.

KATIKA Parokia ya Mtakatifu Imakulata Kanisa Katoliki Upanga jijini Dar es Salaam alipokuwa anasali, Rais Mstaafu Benjamin Mkapa, ameacha alama ya unyenyekevu na kutopenda kujikweza.

Hayo yamebainishwa na Paroko wa parokia hiyo, Padri Casmir Kavishe alipozungumza na HabariLEO ofisini kwake jana mara baada ya Misa ya Kwanza kumalizika.

Gari la Jeshi la Wananchi wa Tanzania JWTZ likiwa limebeba Jeneza lenye mwili wa Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu Marehemu Benjamin William Mkapa wakati likiwasili katika uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam.

Padri Kavishe alisema Mkapa alipenda atambulike kama muumini wa kawaida kama walivyo waumini wengine kanisani hapo na hakutaka cheo chake cha ‘Mheshimiwa Rais Mstaafu’ kitumike katika kumtambulisha au kumuita.

 

“Mkapa alikuwa muumini mzuri na mcha Mungu, kila Jumapili alikuja kanisani na asipoonekana kanisani ilikuwa ama amesafiri au mgonjwa. Alikuwa anawahi kanisani, hakupenda kujikweza, alikuwa mnyenyekevu, alikuwa anakuja na watu wachache kanisani na siyo rahisi kujua kama yupo kanisani,”alisema Padri Kavishe.

Mjane wa Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu Marehemu Mzee Benjamin William Mkapa Mama Anna Mkapa akiwa pamoja na familia yake katika Misa hiyo iliyofanyika katika Uwanja wa Uhuru Jijini Dar es Salaam.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akiwa pamoja na Mkewe Mama Janeth Magufuli wakiwa pamoja na viongozi wengine wa Kitaifa wakishiriki Misa ya Dominika ya 17 ya Mwaka ‘A’ wa Kanisa Katoliki pamoja na Kumuaga Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu Marehemu Benjamin William Mkapa katika Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam.

 

 

Leave a Comment