
SHIRIKA la Fedha Duniani (IMF) limeidhinisha mkopo wa Dola za Marekani Bilioni 4.3 kwa Afrika Kusini ili kuiwezesha nchi hiyo kupambana na janga la virusi vya corona.
Taarifa iliyotolewa na Shirika hilo imesema fedha hizo zinalenga kuisaidia Serikali kukabiliana na mlipuko wa ugonjwa wa COVID-19 unaosababishwa na virusi hivyo pamoja na athari za kiuchumi ambazo zimesababishwa na janga hilo.
Afrika Kusini ambayo ni nchi iliyoathirika zaidi barani Afrika na ni miongoni mwa nchi zenye visa vingi zaidi duniani, imerekodi maambukizi 452,529, vifo 7,067 ambapo 274,925 wamepona.
Wiki iliyopita Afrika Kusini ilipata mkopo wa Rand bil. 5 ambazo ni sawa na Dola mil. 304 kutoka Benki ya Maendeleo Afrika (African Development Bank) ili kusaidia vita dhidi ya virusi hivyo.
Mkopo huo ni wa pili baada ya kupokea mkopo wa dharura wa Dola bil. 1 kutoka New Development Bank mwezi Juni mwaka huu ili kuzidisha nguvu katika fungu maalum la serikali la kuongeza nguvu za uzalishaji mali la R500.