
RAIS John Magufuli amesema rais mstaafu wa awamu ya tatu, Benjamin Mkapa alipenda nyumbani kwao Masasi ndiyo maana alikataa kuzikwa katika eneo lililotengwa jijini Dodoma kwa ajili ya viongozi wa ngazi za juu za serikali.
Magufuli amesema hayo leo Jumatano, Julai 29, 2020, katika Kijiji cha Lupaso, Masasi mkoani Mwtara wakati wa maziko ya Mkapa.
“Tulipangiwa kuzikiwa Dodoma. Mzee Mkapa akaniuliza, ‘Mlipanga maziko yawe Dodoma? Mimi msinizike Dodoma.’ Nikasema, ‘wewe unataka wakuzike wapi?’ Akasema Lupaso. Nikamuuliza Mzee Kikwete akasema ‘mimi mnizike Msoga’. Mimi nilisema nitazikwa Chato.”
“Niliogopa kumuuliza Mwinyi azikiwe wapi kwa sababu alikuwa na miaka zaidi ya 90, nikaona nikimuuliza halafu likatokea la kutokea nitaonekana mimi nimemletea uchuro, nikaona hilo eneo labda atazikiwa Mzee Malecela kwa sababu ni wa hukohuko Dodoma. Kwa sababu hakuna anayetaka kuzikwa Dodoma lile eneo nikaamua kuwapa wananchi na tayari walishaanza kujenga.
“Mkapa alipenda kwao, kwenye hili Watanzania tujifunze, Mzee Mkapa angeweza kuzikwa Dar es Salaam au Lushoto, lakini ndani yake alitaka azikwe mahali alipozaliwa, najua maaskofu mnaniangalia sana kwa sababu ninyi huwa mnazikwa kwenye makanisa,” alisema Magufuli.