
MCHAKATO wa uchaguzi wa kura za maoni ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) umeendelea leo Julai 30, 2020, mwaka huu ili kuwapata wagombea watakaopeperusha bendera ya chama hicho katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 28 mwaka huu.
Jumuiya ya Umoja wa Vijana CCM (UVCCM) nchini wamefanya uchaguzi wa kuwapata wagombea wa uwakilishi wa ubunge viti maalumu, vijana ambapo kwa mkoa wa Kagera uchaguzi huo umefanyika katika ukumbi wa Shule ya Sekondari Bukoba ukiwajumuisha watia nia 19 huku wajumbe halali wa mkutano huo wakiwa 48.
Akitangaza matokeo ya uchaguzi huo, msimamizi mkuu wa uchaguzi ambaye amekuja kwa niaba ya mkuu wa mkoa wa Geita, Said Nkumba, mkuu wa wilaya ya Bukombe amemtangaza Halima Abdallah Bulembo mbunge aliyemaliza muda wake kuwa ameongoza kura za maoni kwa kupata kura 35 akifuatiwa na Joanfaith Kataraia ambaye amepaata kura 9 na Koku Fatuma Ruta ambaye amepata kura 2, Doris Robert kura 1 na Jacrine Elias kura 1 huku wengine waliobaki wakiambulia kura 0.
Nkumba ameongeza kuwa uchaguzi huu ni mchakato wa kura za maoni hivyo mchakato mwingine unaendelea vikiwemo vikao na kuwaasa wagombea wote kushikamana na kutokata tamaa kwa matokeo huku walioongoza wasishangilie maana mchakato bado unaendelea.
Baada ya kutangazwa kwa matokeo, wagombea wote wamepewa nafasi ya kushukuru ambapo wote wameahidi kutoa ushirikiano kwenye uchaguzi mkuu ambao upo mbele yao huku Halima Bulembo akisema kuwa yeye kama mbunge aliyemaliza muda wake na kuendelea kutetea nafasi yake kuwa ataendelea kuwatetea vijana kwenye bunge na kuhakikisha haki za vijana zinapatikana.
Awali akiongea kwenye mkutano huo mkuu wa wilaya Bukoba, Deodatus Kinawiro, amewasihi vijana kutunza nidhamu ya chama na kulinda misingi ya chama chao na kuhakikisha wanashinda katika uchaguzi ujao.
Kinawiro amewataka vijana hao kutotumika vibaya katika uchaguzi huu na kusababisha kujenga picha mbaya ya chama na kuwakemea kutojihusisha na vitendo vya rushwa na kusimamia haki huku wakiwaunga mkono wagombea wote watakaoletwa na chama chao kwenye uchaguzi mkuu.
“Vijana ni jeshi kubwa kwenye chama chetu na ni viongozi wa sasa na viongozi wajao, viongozi wengi mnaotuona tumepikwa kwa kupitia umoja wa vijana sasa itakuwa ni aibu kubwa kumuona kijana wa CCM akijihusisha na vitendo vya rushwa, uvunjifu wa amani na matukio ya hovyo,” amesisitiza Kinawiro.
Aidha amewataka vijana waliowawakilisha vijana wenzao kwenye uchaguzi huu kuwa wawakilishi wazuri na kuwa mfano wa kuigwa kwa vijana wa vyama vingine vya siasa.
Na Allawi Kaboyo Bukoba.