
MSANII wa muziki nchini Uganda, Jackie Chandiru, ambaye aliwahi kupambana na uraibu wa kutumia dawa za kulevya, amerejea tena katika ulingo wa muziki.
Msanii huyo wa kibao kilichotamba cha Golddigger ametoa wimbo mpya kwa ushirikiano na Mkenya, Arrow Bwoy, kwa jina ‘ The One’.
Picha zake akiwa amechanika mwili na huku akikosa kujielewa, zilisambaa kwenye mitandao na vyombo vya habari nchini humo na kuibuka taarifa kwamba alikuwa akitumia dawa za kulevya aina ya cocaine na heroine lakini staa huyo wa zamani wa kundi la Blu 3, amekanusha kuwahi kutumia dawa za kulevya na sasa ameamua kujitosa tena kwenye fani yake ya muziki.
“Nilikuwa mraibu wa kuitumia dawa ya PETHIDINE; ilikuwa dawa ya kupunguza maumivu wala siyo dawa ya kulevya na nilianza kuitumia baada ya kupata jeraha la mgongo ambapo nilifaa kufanyiwa upasuaji ilal ilikuwa ni jambo la 50-50la uwezekano wa kupoteza maisha yangu au kupona.

PETHIDINE ilikuwa dawa ya kunipa afueni ya maumivu haraka na kuanzia mwanzo nilionywa kwamba ningejikuta nimekuwa mraibu wa kuitumia, lakini baadaye nilijikuta katika tatizo la kuacha kuitumia dawa hiyo. Sikuitumia kwa kulewa ama kwa raha, ni kwa sababu nilikuwa naitumia kupunguza maumivu.
“Utumiaji wa dawa hiyo uliathiri taaluma yangu katika muziki na ikafika wakati sikutaka kufanya kazi au kwenda studio, nilitaka tu kuwa peke yangu kwani yalikuwa mambo mengine yaliyojichanganya na nikaanza kupata mawazo mengi kupindukia na wakati watu walipoanza kusema mambo ya kutunga kuhusu mimi niliamua kujifunga kabisa.
“Nafikiri ni jambo zuri lililofanyika kwa sababu nisingekuwa mwanamke ambaye sasa niko hapa, hatua hiyo ilinipa nguvu na kunifunza kwamba watu wanaweza kukuinua na pia wakati mwingine wanaweza kukukanyaga,” alisema Chandiru.
Baada ya madai kwamba anatumia dawa za kulevya, alijaribu kujiua
“…Ndio nilijaribu, sitakanusha hilo nilitaka kujiua, nilikuwa nimechoshwa na kila kitu na hasa habari za uongo katika vyombo vya habari. Kulikuwa na ripoti nyingi kwamba nilikuwa natumia dawa za kulevya ilhali hata sijui cocaine au heroin zinafanana vipi,” alisema Chandiru.