×

Top Five: Wasanii wa Kike Wenye Voko Kali Bongo

Muziki mzuri siku zote hutengenezwa na vitu vizuri ndani yake kwa kuzingatia umakini, mfano melodi nzuri, mashairi na kikubwa zaidi ni sauti.

 

Kwenye ramani ya muziki hapa Bongo kumekuwa na wimbi la wasanii wengi na wenye maajabu yao japo kuna baadhi wanaweza wakawa ni wakali zaidi ya wenzao hasa kwenye upande wa sauti.

Makala haya yanakuletea wasanii wa kike waliojaliwa sauti za kumtoa nyoka pangoni.

 

LADY JAY DEE

Malkia wa muziki wa Bongo Fleva, Judith Wambura ni mwanamuziki mkongwe asiyechuja kwenye gemu tangu miaka ya 2000 mpaka sasa.

 

Lady Jay Dee amebarikiwa sauti ya kipekee ambayo ni ngumu kufananisha na msanii mwingine yoyote kwani aina ya sauti yake ni ile iliyonyooka bila kuwa na mawimbi.

Sauti yake imekuwa ni bora na isiyochuja tangu ameanza kwani mara nyingi imekuwa ikiendana na melodi na aina ya muziki wake.

 

Ngoma kama Siri, Machozi, Teja na nyingine nyingi ambazo ziko ndani ya album zake, zimekuwa ni ngoma ambazo hazichuji kutokana na uzuri wa sauti wa mwanamama huyu.

 

MWASITI

Zao kutokea Nyumba ya Vipaji (THT), Mwasiti Almasi ambaye amekuwa akisifika kuwa na sauti ya kipekee.

Mwasiti ni msanii ambaye sauti yake ina tone ya kitofauti kwenye uimbaji wake kwani amekuwa akijua jinsi ya kuendana na melodi yoyote atakayopewa.

Mwasiti anatikisa na ngoma zake kali kama Sio kisa Pombe, Hao, Perfomance, Kaa nao, Nalivua Pendo na nyingine kibao.

 

LINAH

Estelinah Sanga almaarufu Linah japo wengi wanapenda kumuita ndege mnana na hii ni kutokana na kujaaliwa sauti tamu.

 

Linah ni zao kutokea Nyumba ya vipaji (THT), ambaye amejaaliwa kipaji kikali bila kusahau sauti yake kwani amekuwa ni msanii ambaye anaweza kuimba bila kukwama kama inavyokuwa kwa baadhi ya wasanii. Ametamba na ngoma nyingi kali japo baadhi ni  Lonely, Angalau, Kosa Sina, Atatamani na nyingine kibao.

 

MAUA SAMA

Maua ni msani wa kike ambaye amekuwa akisifika kuwa na sauti kali na ya kipekee. Maua amejaaliwa kuwa na kipaji sana kwenye tasnia ya muziki wa Bongo fleva ikiwemo sauti ambayo iko kwenye mpangilio hata anapokuwa stejini na yuko kwenye chati.

 

Ngoma kama Iokote, Side Chick, Mahaba Niue, Niteke, Amen, Ni wewe na nyingine kali ambazo zinadhihirisha kuwa mrembo huyu ni moto wa kuotea mbali.

 

NANDY

Jina halisi ni Faustina Charles ‘Nandy’ ama African Princess. Ni msanii wa kike ambaye yuko kwenye chati na amekuwa akisifika kuwa na sauti nzuri.

 

Nandy amekuwa akijua kucheza na sauti yake hata anapokuwa stejini kwani ni aina fulani ya sauti ambayo inapanda na kushuka bila kutoka nje ya key.

 

Wasikudanganye, Kivuruge, Ninogeshe, One Day, Haleluyah ni ngoma ambazo amefanya poa sana kwenye mpangilio wa sauti na ziko kwenye chati bila kuchuja kwani mbali na hizo anafanya poa na ngoma ya Acha Lizame ambayo ni moto wa kuotea mbali kila kona unayopita. Wapo wengi wenye sauti nzuri japo hao ni baadhi.

Makala: Happyness Masunga

Leave a Comment