
DAR: Mwanakulitafuta, mwana kulipata! Ndivyo unavyoweza kusema juu ya sakata la video queen (vixen) matata Bongo Anna Kimario ‘Tunda’ kudaiwa kufumaniwa laivu chumbani akiwa na msanii wa Bongo Fleva, David Genzi ‘Young Dee’ wakifanya ‘tabia mbaya’.
Tunda anadaiwa kufumaniwa na mpenzi wake ambaye ni msanii wa Bongo Fleva na Vichekesho, Peter Mlay ‘Whozu’ na kuibuka bonge la timbwili. Ikumbukwe kuwa, mwanaume aliyekuwa naye chumbani (Young Dee), aliwahi kuwa boifrendi wake zamani.
Gazeti la IJUMAA limezungumza na Tunda kutaka kujua ni nini hasa kilijiri ambapo amefunguka tukio lilivyokuwa. Tunda anasema kuwa, Young Dee ni mtu wake wa muda mrefu, lakini pia ni mshikaji wake mkubwa, hivyo alikwenda kwake kisha baadaye walikwenda mazoezini kwa sababu anataka kupunguza uzito.
“Unajua mimi na Whozu siyo wapenzi kivile, tena kama ilivyokuwa zamani.
“Niliamua kwenda zangu kwa David (Young Dee) kwa sababu ni mshikaji wangu na alikuwa mtu wangu.
“Nilipokwenda kwake, alinipeleka mazoezini maana nimeongezeka sana unene,” anasema Tunda ambaye hivi karibuni alidaiwa kutokewa na mapele mwili mzima.
Tunda anaendelea kufunguka kuwa, wakiwa mazoezini huku Young Dee akimfanyisha mazoezi ya kumnyoosha viungo, ndipo alipoibuka Whozu, tena akiwa na nguo ya kulalia na kuibua timbwili la hatari.
“Yaani huwezi kuamini, wakati Young Dee ananifanyisha mazoezi, sijui hata Whozu alitokea wapi, akaanza kufanya fujo, tena amevalia nguo ya kulalia.
“Mimi niliona kama mapichapicha baada ya kumuona akichukua simu ya Young Dee na huwezi kuamini, kwani aliivunja kiasi kwamba haitamaniki kabisa,” anasema Tunda.
Mrembo huyo anasema kuwa, anamshukuru sana Mwenyezi Mungu kwani Whozu hakuligusa gari ya Young Dee lililokuwepo eneo hilo la tukio.
“Ninamshukuru sana Mungu kwa sababu kwa hasira alizokuwa nazo Whozu, sijui nini kingetokea baada ya kuvunja simu, kwani nilijua kinachofuata ni kuvunja vioo vya gari na hapo mambo yangekuwa ni mengi mno,” anasema Tunda ambaye kwa sasa inasemekana amerejesha penzi lake rasmi kwa Young Dee.
Gazeti la IJUMAA lilifanya jitihada za kumpata Whozu, lakini jitihada hizo ziligonga mwamba kwa sababu simu yake iliita bila kupokelewa.
Mbali na Whozu na Young Dee, Tunda aliwahi kutajwa kutoka kimapenzi na wanaume wengi wakiwemo, Diamond Platnumz, Dogo Janja, Casto Dickson, Stan Bakora, Nuh Mziwanda na wengineo.