
KATIBU wa Itikadi na Uenezi (CCM), Humphrey Polepole, wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) ameeleza kusikitishwa kwake na kitendo cha Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kubadili maneno ya moja ya ubeti wa Wimbo wa Taifa wa Tanzania na kuweka maneno ya Chadema wakati wakiimba kwenye moja ya vikao vyao juzi.
Polepole amesema hayo leo Jumatano, Agosti 5, 2020 wakati akizungumza na vyombo vya habari katika Ofisi Ndogo ya Makao Makuu ya CCM (OND) Lumumba Jijini Dar es Salaam.
“Mimi hiki chama nimeshindwa kukielewa, nidhamu ni zero, kutii sheria bila shuruti ni zero, siku wanampokea jamaa yao mgonjwa pale Airport, ilikuwa ni vurugu tupu, wanapita barabara zote, bila kujali wapo watakaotumia barabara hiyo kwenda hospitali na makazini.
“Unawaambia jamani piteni moja hawaelewi, wanapita huku mara kule, wamepita barabara zote na sio kwamba walikuwa wengi, walipofika ofisi zao pale Ufipa wakasema mbona hawajatukamata? Ina maana mpango wao walitaka wakamatwe.
“Kama haikutosha ikaja ya wimbo wa Taifa, bila aibu wanajenga hoja tuambieni wapi tunavunja sheria. Uwe Mmakonde, Msukuma, Mnyaturu, Mnyamwezi, Mkiristo au Muislam ama mshirikina, huu wimbo ni wetu sote, ukisema ‘Sala ya Baba Yetu’ hiyo haichakachuliwi, hata kama baba yako mzazi unampendaje huwezi kusema ‘Baba Yangu Mzazi aliye Mbinguni.’