
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimesema kitawashikisha adabu watia nia waliopenya kwenye kura za maoni za kutafuta wagombea wa Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 28 2020, kupitia chama hicho kwa njia za udanganyifu ikiwemo rushwa.
Hayo yamesemwa na Katibu wa Itikadi na Uenezi (CCM), Humphrey Polepole, wakati akizungumza na vyombo vya habari katika Ofisi Ndogo ya Makao Makuu ya CCM (OND) Lumumba jijini Dar es Salaam, leo Jumatano, Agosti 5, 2020.
“Chama kimeona kiseme, tuko kwenye uchaguzi, mambo ni mengi na muda ni mchache, kila jambo tunalofanya lipo ndani ya katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, tunatambua, kuheshimu na kufuata taratibu na sheria, tamaduni, desturi na taratibu za nchi yetu.
“Tulipenda wote walioomba dhamana wapate nafasi, waende kwenye kura za maoni wakapigiwe kura, viongozi wetu waliopewa dhamana ya kupiga kura wamefanya kazi nzuri sana, kwa uwazi na kwa demokrasia.
“Tunataka viongozi waaminifu, waadilifu wanaochukizwa na rushwa, mwaka huu tutawafundisha watu adabu, wagombea endeleeni kuwa watulivu kabisa, malamiko tunayaruhusu na viongozi wetu wanayapokea, tutawashangaza wanaodhani business as usual (mambo yanakwenda kama kawaida).