
SERIKALI ya Botswana imepiga marufuku uuzwaji wa pombe na kusimamisha leseni za wauzaji wote wa vinywaji. Marufuku hiyo itaendelea mpaka mwongozo mwingine utakapotolewa. Maduka yote ya pombe yatasalia kuwa yamefugwa. Hatua hiyo imekuja ili kuzuia kasi ya maambukizi ya corona.
Wiki iliyopita serikali ya Botswana iliweka amri ya kutotoka nje katika mji wa Gaborone kwa muda wa wiki mbili ili kupunguza maambukizi ambayo yalikuwa yanaongezeka kwa kasi. Taifa hilo limethibitisha kuwa na maambukizi 804 ya homa inayotokana na virusi vya corona — Covid-19 — na vifo viwili.
“Marufuku ya vileo inatokana na ushahidi kwamba unywaji wake huongeza hatari ya watu kukumbwa na Covid-19 kutokana na kutofuata masharti ya kujikinga,” alisema Rais Dkt. Mokgweetsi Masisi.
Hapo nyuma, Botswana ilikuwa imepiga marufuku uuzaji wa vileo wakati ilipotangaza hatua ya watu kutotoka nje.