
Kama kawa mpenzi msomaji wa safu hii ya Yupo Wapi ambayo imekuwa ikikuletea waliowahi kuwa mastaa na kisha kupotea katika tasnia iliyowapa ustaa huo na kuwafanya mashabiki wao wajiulize wapo wapi na wanafanya nini kwa sasa?
Hivyo basi, leo nimekuletea mwanamuziki David Selestine Nyika ambaye jina lake la ustaa ni Daz Baba ambaye alitamba na ngoma kama Namba Nane, Nipe Tano, Elimu Dunia na nyinginezo, pia alikuwa memba wa kundi la Daz Nundaz kuanzia miaka ya 1998 ambapo walitamba na ngoma nyingi kama vile Kamanda, Jirushe na nyinginezo.
Mahojiano ya Paparazi wetu na Daz Baba, yalikuwa kama ifuatavyo;
Risasi: Daz Baba, mashabiki wako wanauliza siku hizi uko wapi na unafanya nini?
Daz Baba: Mimi naishi zangu Tabata hapa Dar, napiga dili zangu kama kawa.
Risasi: Tunajua kwenye muziki sasa hivi siyo kihivyo, sasa hivi unapiga dili gani?
Daz Baba: Sasa hivi napiga dili mbalimbali kama vile biashara ya kuprinti tisheti, uchoraji kwenye majengo na sehemu mbalimbali, pia napiga dili za kutafuta watalii na kuwatembeza sehemu za utalii.
Risasi: Unafikiri ni kwanini ulishuka kimuziki na kuwapa nafasi kina Harmonize, Barnaba, Diamond, Nandy, Ruby na wengineo?
Daz Baba: Kundi kama kundi lilikufa baada ya kila mmoja kuamua kupiga dili zake kivyake alizoona zinamlipa kuliko muziki, lakini mimi kama mimi naweza kusema kilichonishusha ni kukosa menejimenti.
Risasi: Kwahiyo muziki ndiyo basi tena au?
Daz Baba: Siwezi kuacha muziki kwa kuwa uko kwenye damu, na hivi tunavyoongea baada ya kundi la Daz Nundaz kufa, nimeanzisha kundi langu jipya ambalo linaitwa Daz Unit Tanzaniano, ambalo tupo mimi Elvis Sibanda a.k.a Mwenge na washkaji kadhaa.
Risasi: Vipi mmeshaandaa kitu cha kuwarudisha mbele za mashabiki wako?
Daz Baba: Tumeandaa albam yenye nyimbo kumi ikiwemo; Kwanini Ubake, Sauti Zetu, Karibuni Tanzania, Represent na nyinginezo ambazo nawaomba mashabiki wazisubirie kwa hamu.
Risasi: Kipindi mnatamba na Daz Nundaz, najua mlipiga sana pesa, vipi ni kumbukumbu gani ambayo umejiwekea na unapokaa unakumbuka kazi mlizopiga kipindi hicho?
Daz Baba: Kumbukumbu zipo nyingi sana ikiwemo mjengo wangu uliopo Madale hapa Dar, ingawa bado sijaufanyia ‘finishing’.
Risasi: Wewe ni staa wa kitambo, vipi kuhusu familia?
Daz Baba: Bado sijaoa, kuhusu watoto ninao, ila hilo nisingependa kuliweka hadharani sana.
Risasi: Kuna wasanii wenzako; H Baba na Chaz Baba, hawa mna mahusiano yoyote ya kindugu?
Daz Baba: Hapana, ni majina tu yamegongana kama yanavyoweza kugongana majina mengine.
Risasi: Nasikia wewe na Ferouz mna bifu kubwa sana, vipi kuhusu hilo?
Daz Baba: Hilo bifu linakuzwa tu na watu, lakini sisi wenyewe tuko poa kabisa na hata sasa hivi naweza nikampigia usikie tunavyoongea kwa furaha.
Risasi: Sawa Daz Baba, nakutakia kazi njema na ujio wa kundi lako jipya la Daz Unit Tanzaniano.
Daz Baba: Asante sana.
Na Richard Bukos