
SUPER Staa wa Bongo Fleva, Alikiba ambaye pia ni CEO wa Kings Music Records, usiku wa kuamkia leo amefanya bonge moja la shoo katika Uwanja wa Nangwanda Sijaona mjini Mtwara ambako ni nyumbani kwao na msanii mwenzake, Harmonize.
Katika shoo hiyo, Wamakonde walitaka taa zizimwe kisha wakawasha tochi za simu zao za mkononi, hapo ndipo balaa lilipochanganya.
Harmonize ambaye naye ni CEO wa Lebo ya Konde Gang amekuwa akikusanya kijiji wakati akitua kwao Mtwara hasa katika uwanja huo huo wa Nangwanda Sijaona, hivyo Kiba amedhirihisha kuwa yeye bado ni mfalme wa Bongo Fleva kutokana na nyomi alilojaza uwanjani hapo ikizingatiwa kuwa ni shoo kubwa ya kwanza Mtwara tangu msimu wa Corona nchini.
Baada ya shoo hiyo, Kiba anatarajiwa kurejea jijini Dar es Salaam mapema leo kwani kuna mchezo wa hisani wa #NIFUATE kati ya TeamKiba na Team Samatta ambao utachezwa Uwanja wa Mkapa.
Ijumaa Agosti 14, 2020, Alikiba alitarajiwa kuelekea Kigoma kwa ajili ya shoo yake nyingine kubwa mkoani humo.