
MATUKIO ya watu sehemu mbalimbali nchini kudaiwa kufa na baadaye kupatikana wakiwa hai ‘kufufuka’, yanazidi kuzua utata miongoni mwa jamii, Risasi Jumamosi lina mkasa mpya.
Katika hali isiyokuwa ya kawaida, wakazi wa Kijiji cha Darajani, Kata ya Inyala, Wilaya ya Mbeya, mkoani Mbeya, Agosti 3, mwaka huu, walishikwa na taharuki baada ya mwanaume mmoja kukutwa kwenye shamba la viazi na kudaiwa ni msukule.
Yusuph Khamis ni mmoja wa mashuhuda wa tukio hilo alisema, walimkuta mtu huyo akiwa mtupu huku akishindwa kujieleza alifi kaje eneo hilo akiwa kwenye hali hiyo na kuzua utata miongoni mwa mashuhuda.
“Alikuwa ametapakaa mchanga mwili mzima kama mtu aliyefukuliwa ardhini, watu walimuogopa.
“Kitu kingine cha kustaajabisha, huyo jamaa sehemu zake za siri zilikuwa za kiume, lakini kifuani alikuwa na matiti kama mwanamke,” alisema Yusuph kwa mshangao.
Aliongeza kuwa, baadaye wananchi walimstiri mwanaume huyo kwa mavazi na kisha kumpeleka Kituo cha Polisi Inyala ambako alishindwa kuhojiwa kwa kile kilichotajwa kuwa ni kutoweza kuzungumza.
Wakati hali hiyo ikijitokeza kituoni hapo, alijitokeza mwanaume mwingine anayedaiwa kuwa ni mchungaji wa kanisa (halikutajwa), ambapo aliwaomba polisi mtu huyo ili akamfanyie maombi.
Baada ya ombi la mchungaji huyo aliyejitambulisha kwa jina na Clemence Nchimbi, kukubaliwa na polisi, aliondoka na mwanaume huyo hadi kanisani kwake kumuombea.
Hata hivyo, baadaye zilivuja taarifa kutoka kwa mchungaji kuwa mwanaume huyo ‘msukule’ ameweza kuzungumza na kujitambulisha kwa jina la Edward Dickson.
Kwa mujibu wa mchungaji, Edward alidai kuwa ametokea nchini Zambia na kudai kuwa amewahi kufa na kisha kufufuka, jambo ambalo ni tata.
Inaelezwa na mchungaji huyo kwamba, mwanaume huyo hajaweza kupata ufahamu kamili, kwani kuna wakati alidai kuwa amewahi kuishi hapa nchini maeneo mbalimbali kabla ya kufa na kufufuka.
Matukio ya watu kufa na kudai kufufuka, yamekuwa yakizua utata, kwani yamejaa nadharia ambayo haijapata mashiko kitaalamu kutokana na kukosa uthibitisho.
Mwishoni mwa mwaka jana, eneo la Ilula mkoani Iringa, mwanamke aitwaye Kabula Masunga alikutwa juu ya paa la nyumba ya mchungaji akidaiwa kudondoka usiku katika harakati zake za kichawi, lakini baadaye ikajulikana kuwa mwanamke huyo alilipwa fedha ili ‘kupromoti’ huduma ya mchungaji aliyetajwa kwa jina la Jeremiah Charles.
STORI: EZEKIEL KAMANGA, RISASI