×

Azam FC Wataja Dau Wanalolitaka Yanga SC Kwa Sure Boy

MATAJIRI wa Azam FC, wamekubali kumuachia kiungo wao mchezeshaji fundi, Salum Abubakary ‘Sure Boy’ kwenda kuichezea Yanga kwa dau la Sh 40Mil kwa misimu miwili.

 

Hiyo ikiwa ni siku chache tangu uongozi wa Yanga upeleke barua ya maombi ya kuhitaji huduma ya kiungo huyo mwenye uwezo mkubwa wa kupiga pasi za mwisho za kufunga mabao katika msimu ujao.

 

Yanga imedhamiria kutengeneza timu itakayokuwa na ushindani mkubwa katika msimu ujao, ikiwemo kuchukua mataji yote watakayoyashindania.

 

Kwa mujibu wa taarifa ambazo imezipata Championi Jumamosi, Yanga imepeleka Azam ofa ya Sh 20Mil kwa ajili ya kumnunua kiungo huyo aliyeomba mwenyewe kuondoka na kwenda kutafuta changamoto sehemu nyingine.

Mtoa taarifa huyo alisema dau hilo la usajili wamelikataa Azam na kuomba waongeze na kufikia Sh 40Mil ili asaini mkataba huo wa kwenda kuichezea timu hiyo.

 

“Yanga wamepeleka barua ya kumuhitaji Sure Boy, lakini uongozi wa Azam wanajadiliana juu ya ofa ndogo ya Sh 20Mil waliyoipeleka ambayo wamesema ni ndogo huku wakipanga kuwajibu.“Uongozi wa Azam umesema kuwa thamani ya Sure Boy siyo ya Sh 20Mil, yeye thamani yake ni 40Mil, hivyo Yanga kama wanamuhitaji basi wamuongee dau ili wamuachie,” alisema mtoa taarifa huyo.

 

Alipotafutwa Ofisa Mtendaji Mkuu wa Azam, Abdulkarim Amin ‘Popati’ kuzungumzia hilo alikiri kupokea ofa hiyo kwa kusema: “Ni kweli Yanga wamewasilisha barua pamoja na ofa yao ya kumuhitaji Sure Boy.

 

“Hivi sasa tupo kwenye kikao, lakini muda siyo mrefu tutawajibu juu ya ofa yao, lakini nichukue nafasi hii kuwapongeza Yanga kwa kufuata taratibu za usajili, walianza kwa Nchimbi (Ditram) ambaye walimuhitaji na kumuachia kwenda huko.”

Leave a Comment