
UMATATU iliyopita, Yanga ilitangaza kuachana na wachezaji wake ambao wengi wao mikataba yao imemalizika.
Wachezaji walioachwa ni Mrisho Ngasa, David Molinga, Jaff ary Mohamed, Tariq Seif, Andrew Vicent, Papy Tshishimbi, Mohamed Issa, Kelvin Yondani na Juma Abdul.
Wengine ni Ally Mtoni, Muharami Issa, Yikpe Gislain, Ali Ali, Patrick Sibomana, Eric Kabamba na Raphael Daud.
Baada ya kuachana na nyota hao, ipo kwenye hatua za mwisho kumalizana na nyota wengine wa ndani na wa kimataifa, kisha kuwatambulisha.
Baadhi ya nyota hao ni Eric Rutanga raia wa Rwanda, Tuisila Kisinda na Mukoko Tonombe, wote raia wa DR Congo, huku Kibwana Shomary akiwa kwenye rada zao pia.
Mpaka jana Jumamosi mchana, Yanga ilikuwa imemalizana na nyota wanne ambao imewatambulisha tayari, huku wakisubiri msimu wa 2020/21 uanze, wakichafue uwanjani.Nyota hao ni beki wa kushoto Yasin Mustafa kutoka Polisi Tanzania, mshambuliaji Waziri Junior (Mbao), beki wa kati Bakari Mwamnyeto (Coastal Union) na kiungo mkabaji Zawadi Mauya kutoka Kagera Sugar.

Wakati usajili ukiwa unaendelea, Ofi sa Muhamasishaji wa Yanga, Antonio Nugaz, amesema: “Wanayanga wasitiwe unyonge, wasubiri anga lifunguliwe Agosti 15 wataona vifaa vya kimataifa vinashuka pale uwanja wa ndege.“Tunakwenda kutengeneza kikosi tishio, kishindo cha wakimataifa kinakuja kwa kasi.
Wanayanga watafurahi wenyewe.”Kesho Jumatatu, kikosi cha Yanga kinatarajiwa kuingia kambini na kuanza maandalizi ya msimu ujao, huku pia Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) ikisema kesho hiyohiyo itaweka hadharani ratiba ya Ligi Kuu Bara 2020/21.
Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Ligi, Almas Kasongo, amesema: “Mchakato wa kuandaa ratiba ya msimu wa 2020/21 unaelekea ukingoni kukamilika.
Tunaamini Agosti 10 kila kitu kitakuwa tayari, hivyo tutaiweka hadharani.“Pia kuanzia msimu wa 2020/21, tumepanga kuwa na kombe maalum la ligi ambalo litakuwa linakabidhiwa kwa washindi tofauti na ilivyokuwa misimu ya nyuma kwamba makombe yanatofautiana kila msimu.
Tunataka watu wakiliona kombe wajue kabisa hili ni la Ligi Kuu Bara, tumeamua kufanya hivyo ili kuondoa mkanganyiko.”
JESHI LA YANGA
Yanga baada ya kuachana na nyota wake, kisha kusajili wapya, mpaka sasa jeshi lao la msimu ujao lipo hivi;
MAKIPA: Farouk Shikalo, Metacha Mnata na Ramadhan Kabwili.
BEKI WA KULIA: Paul Godfrey.
MABEKI WA KUSHOTO: Yasin Mustafa na Adeyum Saleh.
MABEKI WA KATI: Lamine Moro, Said Juma Makapu, Bakari Mwamnyeto na Abdallah Shaibu ‘Ninja’.
VIUNGO WAKABAJI: Zawadi Mauya, Feisal Salum ‘Fei Toto’ na Abdulaziz Makame.
VIUNGO WASHAMBULIAJI:Haruna Niyonzima, Balama Mapinduzi, Deus Kaseke na Juma Mahadhi.
WASHAMBULIAJI: Wazir Junior na Ditram Nchimbi.