
MSIKITI mkubwa wa kisasa wa ghorofa mbili ambao utakuwa Msikiti wa Wilaya ya Kisarawe mkoani Pwani unatarajiwa kugharimu zaidi ya Sh.milioni 500 huku Mkuu wa wilaya hiyo Jokate Mwegelo akiahidi kusimamia ujenzi wa msikiti huo na utakamilika ndani ya mwaka mmoja.

Jokate ambaye ameombwa kuwa mlezi wa Msikiti huo wa Wilaya ya Kisarawe amewahakikisha waumini wa dini ya Kiislamu wilayani hapa kuwa anaamini hakuna kinachoshindikana na tayari ameanza kuzungumza na wadau wa ndani na nje ili kusaidia ujenzi huo na kwamba msikiti huo ukikamilika utakuwa umebeba taaswira ya wilaya hiyo ya Kisarawe.

Akizungumza na waumini wa dini hiyo wilayani hapa, Jokate Mwegelo amesema katika maisha yake hakuwa akifikiria kuna siku moja atapa heshima ya kuwa mlezi wa msikiti na kuombwa kushiriki kikamilifu kwenye ujenzi wa msikiti lakini wananchi wa Kisarawe wamempa heshima hiyo ambapo amesisitiza hatawaangusha na atashirikiana nao bega kwa bega hadi msikiti ukamilike.

“Nimefurahi sana kwa heshima kubwa mliyonipa ya kuwa mlezi wa kamati yenu ya ujenzi yenye kuratibu shughuli za ujenzi wa msikiti wa Islamiya Kisarawe na niseme kwa dhati ya moyo wangu ahsante sana, nimeridhia kuwa mlezi na kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu jinsi atakavyotuongoza naaamini sitowaangusha.Tutafanikisha ujenzi wa msikiti wetu huu wa Wilaya ya Kisarawe ambao utakuwa taaswira ya misikiti mingine ndani ya Wilaya yetu.

“Sisi sote tunafahamu msikiti ni taasisi inayojishughulisha na mambo mbalimbali ya kimaisha katika jamii ni pamoja na shughuli za maendeleo,kiuchumi na kiutamaduni na kwa mantiki hiyo kuwa na jengo la msikiti ni jambo muhimu katika kuratibu utekelezaji wa shughuli hizo,”amesema Jokate Mwegelo.

Amefafanua anaungana nao katika juhudi zote za ujenzi wa msikiti huo wa Kisarawe na atakuwa nao mguu kwa mguu, bega kwa bega hadi ujenzi ukamilike huku akisisitiza shughuli za uchumi na huduma ambazo zitakuwa zinatolewa na msikiti huo zitasaidia katika kupambana na umasikini, ujinga na maradhi , hivyo wananchi na taifa kwa ujumla litasonga mbele.

Amesema hata maandiko matakatifu ya Quraan yanaeleza Mwenyezi Mungu humpenda mja wake anayejituma katika kufanya kazi, hivyo akiwa mlezi wa kamati iliyoundwa kushughulikia ujenzi atajitajidi kadri Mungu atakavyomuwezesha kutoa mchango wake wa hali na mali kufanikisha ujenzi huo mkubwa na wa kihistoria, pia ameahidi atashirikiana na waumini wote, wadau wote na marafiki wote kuujenga msikiti wa Wilaya ya Kisarawe.

“Pamoja na kuzungumzia ujenzi wa msikiti huu, sote tunafahamu kwamba tuko kwenye kipindi cha kuelekea uchaguzi mkuu unaotarajia kufanyika Oktoba 28, 2020,hivyo nitoe rai kwenu Kisarawe, dini zote na wananchi wote kuzingatia amani na utulivu.Sitarajii uvunjifu wa amani ndani ya Wilaya ya Kisarawe.
“Na nimesema hivyo nikiamini viongozi wa dini ndio walezi wetu , ndio viongozi wetu wa dini ambao mko karibu na jamii, tuwasaidie vijana watulie, uchaguzi ufanyike kwa usalama na kisha tuendelee na majukumu yetu ya kuijenga Kisarawe.Mpaka tumefika hapa tayari Mungu ametufanyia wepesi tutaujenga msikiti huu huku tukiendelea kuwa watulivu,”amesema Jokate Mwegelo.

Amewaomba waumini wa dini hiyo na viongozi wa dini zote kwa ujumla kumuendelea kumuombea Rais Dk.John Magufuli ili aendelee kuwa mwenye afya njema na kuijenga nchi yetu kwa kuiletea maendeleo.
Awali akisoma risala kuhusu ujenzi wa msikiti huo, Katibu wa Msikiti wa Wilaya ya Kisarawe Mohamed Bakari amesema kwamba wazo la kuujenga msikiti huo ili uwe mkubwa wa kisasa lilianza mwaka 2000, na eneo lilipatikana mwaka 2006 na ilipofika mwaka 2007 wakapata ramani na ujenzi ukaanza mwaka 2018.

“Tulianza kuchanganishana fedha kupitia michango ya waumini wetu na katika kipindi cha miaka 10 tukafanikiwa kukusanya Sh.milioni 45 lakini ili msikiti huu ukamilike kama ramani ilivyo tunahitaji kupata zaidi ya Sh.milioni 500.
“Hivyo Mkuu wa Wilaya tunaomba nguvu yako ili tuungane pamoja kufanikisha dhamira hii ya waumini wa dini ya Kiislamu wa Kisarawe kuwa na msikiti mkubwa wa kisiasa,”amesema Sheikh Bakari.