
KLABU ya Juventus imemteuwa mchezaji wao wa zamani Andrea Pirlo kuwa kocha wa timu hiyo, saa chache baada ya Maurizio Sarri kutimuliwa. Pirlo 41, amesaini mkataba wa miaka miwili hadi 2022.
Kiungo huyo wa zamani wa Italia siku 9 zilizopita alipewa jukumu la kuwa kocha wa timu ya vijana chini ya miaka 23 kwenye klabu hiyo, ajira ambayo ameitumikia kwa siku tisa tu kabla ya kupandishwa lakini hivi sasa Andrea Pirlo amethibitishwa rasmi kama mrithi wa mikoba ya Maurizio Sarri.
Akiwa na Juventus ameshinda ubingwa wa Kombe la Dunia 2006 akiwa na Italy, Bingwa wa Serie A mara sita, baada ya kushinda mbili na Milan na mara nne akiwa na Juve. Alishinda ndoo mbili za Ligi ya Mabingwa akiwa na Milan, 2003 na 2007. Bingwa wa Coppa Italia mbili na Italia Super Cup.
Wengi wameshangazwa na uteuzi huu ambapo walifikiri kuwa Juventus wangetafuta kocha mwenye uzoefu wa hali ya juu kwa timu kubwa namna hiyo.Juventus ambayo ina wachezaji mastaa kama Cristiano Ronaldo, iliondolewa kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya wikiendi iliyopita na muda mchache baadaye ikamtimua Sarri.
Awali Juventus ilikuwa inatajwa kuwa ingeweza kumchukua kocha wa sasa wa Real Madrid, Zinedine Zidane au kocha wa zamani wa Tottenham, Mauricio Pochettino ambaye hana kazi.