




Mwanafunzi wa sekondari umri wa miaka 17 Rannia Nasser amezindua maonesho ya picha maarufu kama ‘WATU WA TANZANIA’ yanayofanyika katika ukumbi wa Alliance Francie na kudhaminiwa na Ubalozi wa Ufaransa kwa siku tano mfululizo yaliyoanza Agosti 7 hadi 12 mwezi huu lengo ikiwa ni kusaidia kukuza utalii nchini kutokana na picha hizo kubeba maudhui yanayoonesha shughuli mbalimbali za kiuchumi pamoja na maisha halisi ya mtanzania yaliyojaa simulizi na historia za Taifa letu.
Akizindua maonesho hayo rasmi Naibu Waziri wa Mambo ya Nje Dkt. Damas Ndumbaro kwa niaba ya Serikali ya Tanzania aliahidi kuendelea kuimarisha mahusiano ya Kidemokrasia na kiuchumi kati ya Serikali ya Tanzania na Serikali ya Ufaransa ikiwa ni pamoja na kutumia mahusiano hayo katika kuitangaza Sekta ya utalii iliyopo nchini ili sekta hiyo iweze kutangazika zaidi katika mataifa mbalimbali ulimwenguni.
Amesema “Tanzania na Ufaransa tunamahusiano mazuri kwa muda mrefu hali ambayo kwa kiasi kikubwa inatunufaisha nchi zote kwenye nyanja mbalimbali hivyo ni wajibu wetu kama nchi kuyatunza mahusiano haya ili yanendelee kutunufaisha”.
Pia mara Baada ya kuzindua Maonesho hayo Ndumbaro alipongeza mwanafunzi Rannia Nasser kwa jinsi alivyojitoa muda wake na kupiga picha nzuri zinazoonesha uhalisia na jinsi watanzania tunavyoishi kwa upendo Amani na kuamua kuzitoa bure picha zote kwa Bodi ya Utalii Tanzania ili zitumike kukuza utalii nchni.
“Hongera sana Rannia kwa niaba ya watanzania wote ninakushukuru” alisema Ndumbaro. Naibu Waziri Wizara ya Mambo ya Nje.
Naye Balozi wa Ufaransa nchini Tanzania, Frederic Clavier kwa nafasi yake pamoja na mambo mengine ameahidi kuendelea kuzitangaza fursa za utalii zilizopo Tanzania ili sekta hizo ziendelee kuimarika na hatimaye kukuza uchumi wa Taifa.
“Sisi Ufaransa tutaendelea kushirikiana na Tanzania ili kila ubunifu unaolenga kuimarisha utalii uweze kuleta maendeleo nchini.” alisema Balozi wa Ufaransa.
Mkurugenzi wa Bodi ya Utalii Tanzania TTB Bi Devotha Mdachi aliahidi kuziweka picha hizo katika vivutio vya utalii nchini vilivyopo nchini na kubanisha kuwa sanaa hii ya picha ambayo imepewa jina la Watu wa TANZANIA wataiendeleza kwa kuwa itasaidia mataifa mengi ulimwenguni kufahamu uhalisia wa maisha ya watanzania vyema na kukuza Utalii.