
KUMEKUWA na mwitikio mkubwa kwa waajiri waliofika kwenye banda la Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) kutaka kujua jinsi ya kujisajili na kuwasilisha madai ya fidia kupitia mtandao yaani Online Registration System-WCF Portal (ORS), Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko huo Bw. Masha Mshomba amesema.
Bw. Mshomba ameyasema hay leo (Agosti 8, 2020) kwenye banda la Mfuko huo katika maonesho ya Nanenane yanayofanyika kwenye viwanja vya Nyakabindi Mkoani Simiyu.
“Imekuwa ni nafasi nzuri sana ya mfuko kuelezea huduma zake hususan huduma mpya ambazo zinapatikana kupitia mtandao zinaanzia katika hatua ya mwanzo kabisa ambayo mwajiri anataka kujisajili katika mfuko, kuleta michango kupitia mtandao lakini kubwa zaidi ni jinsi ya kutoa taarifa (kuwasilisha madai) endapo mfanyakazi amepata ajali au ugonjwa utokanao na kazi.” Alisema Bw. Msomba.
Alisema katika maonesho hayo waajiri wengi walifika katika banda la WCF wakiwa na shauku kubwa ya kuelewa jinsi ya kujisajili na kuwasilisha madai kupitia mtandao.
“Tumepata mwitikio mzuri sana karibu waajiri 200 wamefika kujisajili kupitia mtandao nah ii inaonyesha ni jinsi gani suala la matumizi ya mtandao limerahisisha sana utoaji wa huduma za mfuko na hii inakwenda sambamba na azma nzima ya serikali yetu inayoongozwa na Mhe. Rais Dkt. John Pombe Magufuli ambaye anatamani sana kuona taasisi hizi za serikali zikitumia huduma hizi za mtandao kwasababu anajua wazi kwamba zinapunguza gharama na zinaleta ufanisi katika utendaji wa taasisi na taifa zima kwa ujumla.” Alisisitiza.
Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi ni taasisi ya serikali yenye jukumu kubwa la kulipa fidia kwa mfanyakazi aliyeumia, kuugua au kufariki kutokana na kazi na walengwa hasa ni watumishi wote kutoka sekta ya Umma na Binafsi Tanzania bara.
Na mwandishi wetu, Simiyu Agosti 8, 2020