KIUNGO mchezeshaji fundi wa Azam FC, Salum Abubakary ‘Sure Boy’, anatarajiwa kuigharimu Yanga jumla ya Sh milioni 161 ukiachana na posho na marupurupu mengine katika mkataba wake wa miaka miwili Jangwani.
Nyota huyo hivi karibuni aliandika barua ya kuomba kuondoka Azam baada ya kuitumikia kwa kipindi cha miaka 13 tangu alipojiunga nayo ikiwa Daraja la Kwanza.
Azam na Yanga hivi sasa zipo kwenye mazungumzo ya mwisho kwa ajili ya kukamilisha dili hilo la usajili katika kuelekea msimu mpya wa 2020/2021 uliopangwa kuanza Septemba 6, mwaka huu.
Kwa mujibu wa taarifa ambazo imezipata Championi Jumatatu, kiungo huyo anatarajiwa kuchukua dau la usajili la Sh 45Mil, mshahara wa Sh 4Mil kila mwezi na na fedha ya kuvunja mkataba watakayopewa Azam ni Sh 20Mil..
Dau hilo la usajili la Sh 45Mil ukijumlisha na fedha ya kuvunja mkataba wa mwaka mmoja Azam inakuwa Sh 65, na Sh 96Mil za mshahara atakaouchukua Yanga kwa kipindi cha miaka miwili, jumla ataigharimu timu hiyo Sh milioni 161.
Taarifa kutoka kwa chanzo chetu makini cha habari zinasema kuwa timu hizo mbili zilitarajiwa kumalizana juzi Jumapili. Na jana Jumatatu, kiungo huyo anatarajiwa kutambulishwa rasmi kama mchezaji wa Yanga.
Mtoa taarifa wetu alidai kuwa Sure Boy aliomba kuondoka Azam kutokana na mshahara mdogo anaoupata wa Sh 2Mil kwa mwezi wakati Yanga wakimuongezea mara mbili ya fedha hizo.
“Sure Boy amelazimisha kuondoka Azam kutokana na kiwango kidogo cha mshahara anachochukua na kingine mapenzi aliyonayo Yanga kwa kipindi kirefu.
“Tangu muda mrefu Sure Boy alikuwa na ndoto za kuichezea Yanga, hiyo nayo ni sababu kubwa na ndiyo maana kaandika barua ya kuomba kuondoka.
“Yanga wamemuwekea dau la usajili la Sh 45Mil atakazozichukua kwa kipindi cha miaka miwili, siyo nyingi lakini mshahara ndiyo mkubwa ambao ni mara mbili ya aliokuwa anachukua Azam,” alisema mtoa taarifa huyo.
Ofi sa Mtendaji Mkuu wa Azam, Abdulkarim Amin ‘Popati’ juzi alizungumzia hilo na kukiri kupokea ofa hiyo kwa kusema: “Ni kweli Yanga wamewasilisha barua pamoja na ofa yao ya kumhitaji Sure Boy.
“Hivyo basi hivi sasa tupo kwenye kikao, lakini muda siyo mrefu tutawajibu juu ya ofa yao, lakini nichukue nafasi hii kuwapongeza Yanga kwa kufuata taratibu za usajili, walianza kwa Nchimbi (Ditram) ambaye walimhitaji na tukamuachia kwenda huko.”
WILBERT MOLANDI, Dar es Salaam.
