MWANAMUZIKI wa Bongo Fleva na mjasiriamali, Zuwena Mohammed ‘Shilole’ au ‘Shishibaby’ ameamua kuvunja ukimya na kuanika kwamba tangu akiwa mdogo hakuwahi kumjua baba yake mzazi kwani aliondoka akiwa anatambaa.
Shilole ameanika hayo jana Jumatano, Agosti 12, 2020, usiku wakati akifanya mahojiano na Clouds TV kuzungumzia maisha yake na namna alivyopambana mpaka kufika hapo alipo leo.
“Mama aliniambia baba yangu aliondoka nikiwa natambaa, hakurudi tena sasa hadi hakikisha miaka saba sikuwahi kumuona baba, hadi mama anafariki sikuwahi kumuona baba, sikuwahi kupata historia yoyote kuhusu baba.
“Niliambiwa kuwa baba yangu yupo ila sijawahi kumuona anaitwa Mzee Mohammed Yusuf, nimekuja kujua juzi tu kama miaka mitatu iliyopita. Wababa wengi wameibuka wanasema mimi mtoto wao.
“Nilikuwa na ndoto za kuwa pilot, nilikuwa nina ndoto za kurusha ndege Marekani, yule mwanaume wa kwanza aliyenipa ujauzito aliniharibia ndoto zangu, ” amesema Shilole.
Aidha, Shilole amesema kuwa ana tamani siku moja aje kuwa kiongozi kwenye Taifa hili la Tanzania ili awasaidie wanawake na watoto wanaonyanyaswa.
