×

Hatimaye Willian Atua Arsenal

KLABU ya Arsenal imemsajili kiungo wa kati wa Brazil, Willian kwa mkataba wa miaka mitatu baada ya mkataba wa mchezaji huyo, 32, kukamilika. The Blues ilitoa ofa yake mpya kwa mchezaji huyo lakini haikuwa tayari kufikia kile ambacho the Gunners imempa.

 

“Naamini ni mchezaji ambaye kweli anaweza kutufanyia mabadiliko makubwa. Tulikuwa tumedhamiria kabisa kuimarisha upande wa kushambulia wa kuingo wa kati na nafasi ya winga,” amesema kocha wa Arsenal Mikel Arteta.

Willian alishiriki michezo 339 kwa Chelsea baada ya kusajiliwa kutoka klabu ya Anzhi Makhachkala ya Urusi kwa pauni milioni 30 mwaka 2013.

 

“Ni mchezaji ambaye tunaweza kumbadilisha badilisha, Anaweza kucheza nafasi tatu au nne tofauti. Ana tajriba ya kila safu ya uwanja wa soka lakini bado ana nia ya kuja hapa kuchangia kuweka klabu katika nafasi inayostahili kuwa,” Arteta ameongeza.

 

“Nimefurahishwa sana na mazungumzo yangu nae na jinsi alivyokuwa anataka kujiunga nasi.”
Arsenal ilimaliza ya nane katika Ligi ya Premia msimu uliopita, huku Chelsea ikimaliza ya nne na kupata nafasi ya kushiriki katika kombe la klabu bingwa Ulaya.

Hata hivyo, Gunners iliwashinda mahasimu wao wa Uingereza katika fainali ya kombe la FA mechi ambayo Willian hakucheza kwasababu ya jeraha – ili kuhakikisha inajipatia nafasi katika mechi za Ligi ya Ulaya. Willian anafuata nyayo za mlinzi David Luiz aliyehama Chelsea na kujiunga na Arsenal Agosti mwaka jana.

 

Mkurugenzi wa kiufundi katika klabu ya Arsenal Edu alisema: “Namfahamu vizuri sana, kwa kipindi kirefu kwasababu tumekuwa tukifanyakazi pamoja katika timu ya taifa ya Brazil. Anasifa nyingi nzuri yeye binafsi na pia kama mchezaji wa kandanda.”

Leave a Comment