TIMU ya soka ya wanawake ya Simba Queens, juzi Jumatano walikabidhiwa ubingwa wao wa Ligi Kuu ya Wanawake ambapo sherehe hizo zilitanguliwa na mchezo wa kumaliza ligi baina ya Simba na TCS Queens ambapo Simba walifanikiwa kuibuka na ushindi wa mabao 9-0 kwenye Uwanja wa Nyamagana jijini hapa.
Mara baada ya mchezo huo, Kocha Mkuu wa Simba Queens, Mussa Mgosi alisema: “Haikuwa kazi rahisi kwetu sisi Simba kutwaa ubingwa huu, kama mnavyojua tumesota kwa zaidi ya miaka mitatu sasa lakini tumefanikiwa, nawapongeza sana wachezaji wangu.
“Uongozi mzima wa bodi ya wakurugenzi wa Simba malengo yake ni kuhakikisha kwamba tunatawala soka la Tanzania kuanzia timu ya wanaume na timu ya wanawake, kwa mwaka huu tumeweza kufanya hivyo, kimsingi hatutabweteka.”
Simba Queens baada ya kutwaa ubingwa huo watajipatia zawadi ya fedha Sh milioni 15, huku JKT Queens ambao wameshika nafasi ya tatu watajipatia zawadi ya Sh milioni 10 na Alliance ambao wamemaliza nafasi ya tatu wakiambulia Sh milioni 5