×

Kwa Chama Hili Mnatokaje

MNASIKIA au tuongeze sauti? Ndivyo wanavyouliza mashabiki wa Simba kufuatia kufanya usajili wa kufuru waliofanya mpaka sasa na wakijiuliza kwa chama walilonalo mnatokaje?

 

Simba imeshusha vifaa vya hatari kwa ajili ya msimu ujao mpaka sasa huku baadhi ya wachezaji wakiingia moja kwa moja kwenye kikosi cha kwanza kitakachokuwa chini ya Mbelgji, Sven Vandenbroeck kwani wamepania kufanya makubwa.

 

Tayari Simba imeshusha Mghana, Bernard Morrison ambaye uwezo wake unajulikana akitokea Yanga lakini wamemchukua beki katili kutoka Gor Mahia ya Kenya, Joash Onyango kabla ya juzi kumtambulisha kiungo fundi, Mzambia, Larry Bwalya.

 

Simba hawakuishia hapo katika upande wa ushambuliaji wamefanikiwa kumuongeza Cris Mugalu raia wa DR Congo ambaye alikuwa akikipiga katika Klabu ya Power Dynamo ambaye alitangazwa jana huku kwa upande wa wachezaji wa ndani wakiwa ni Ibrahim Ame (Coastal Union), David Kamenta (Lipuli) na Charles Ilanfya wa KMC.

 

Timu hiyo ambayo inakwenda kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika inatarajia kuwa na sura mpya za mastaa katika kuhakikisha wanasaka rekodi yao ya kutinga hatua ya robo fainali msimu wa 2018/19 na ikiwezekana kulitwaa kombe hilo kabisa.

 

Kikosi cha timu hiyo ambacho kitakuwa moto, kinatarajia kuanza na kipa Aishi Manula ambaye ndiye kipa bora wa msimu huu hali inayopelekea kuendelea kumuweka benchi Beno Kakolanya.

 

Licha ya uongozi kumshusha Duchu lakini uwezo mkubwa umeendelea kumbakisha beki wa kulia, Shomari Kapombe katika kikosi hicho sawa na nahodha msaidizi Mohamed Hussein ‘Tshabalala’ anayecheza nafasi ya beki wa kulia kuendelea kubakia.

 

Katika nafasi ya beki wa kati kwa namba nne na tano kutakuwa na sura mpya ambazo ni Ibrahim Ame na beki wa kimataifa Joash onyango.

 

Jonas Mkude ‘Nungungu’ akiendelea kutesa katika nafasi ya kiungo mkabaji akisaidiana na fundi mpya kutoka Zambia, Larry Bwalya katika kuanzisha mashambulizi.

 

Luis Miquissone yeye atakuwa akitokea winga ya kulia sambamba na Morrison atakayekuwa akitokea kushoto katika kushambulia wakati Clautous Chama ‘ Mwamba wa Lusaka’ akiwa anasimama namba kumi kuhakisha mshambuliaji mpya ambaye ameenda hewani Mcongo, Cris Mugalu akifanya kazi moja tu ya kutupia mabao ya uhakika.

 

Simba wamedhamiria kufanya kweli Afrika na wameshajinasibu kuwa kwenye ligi ya Bongo wanatakwa kutwaa ubingwa mara kumi mfululizo. Sasa wameshatwaa mara tatu mfululizo.

Imeandikwa na: Ibrahim Mussa, Joel Thomas na Lunyamadzo Mlyuka.

Leave a Comment