RAIS wa Mali, Ibrahim Boubacar Keïta, amejiuzulu muda mfupi baada ya kuwekwa kizuizini na jeshi la nchi hiyo. Akilihutubia taifa kwa njia ya televisheni, Keïta amesema anaivunja serikali na bunge.
“Sitamani damu imwagike ili nisalie madarakani,” Keita alisema. “Nimeamua kujiuzulu kutoka kwenye nafasi yangu.”
Hatua hii imekuja saa kadhaa baada ya kiongozi huyo wa juu na Waziri Mkuu Boubou Cissé kupelekwa kwenye kambi ya jeshi karibu na mji mkuu Bamako, hatua iliyosababisha mataifa ya Afrika Magharibi na Ufaransa kulaani kitendo hicho.
”Ikiwa leo, sehemu ya vikosi vilivyo na silaha wanataka hili liishe kwa kuingilia kati, nina cha kufanya?” alisema Keïta.
Rais huyo pamoja na waziri mkuu wake walikamwatwa na jeshi baada ya maandamano yaliyodumu kwa miezi kadhaa kumtaka Keita kung’atuka madarakani.
Keita ambaye alikuwa katika muhula wake wa pili wa uongozi alikuwa akituhumiwa kusababisha mdororo wa kiuchumi nchini humo pamoja na kushindwa kuyazuia makundi ya wapiganaji wa Kiislamu ambayo yameharibu amani ya nchi hiyo.
