×

Darey arejea na Jah Guide Me

 

MKALI wa muziki wa Afro Beat, Mnigeria Dare Art Alade a.k.a Darey, baada ya kimya cha miaka minne amerejea na singo mpya inayokwenda kwa jina la ‘Jah Guide Me’ ambayo tayari inapatikana pia kwenye video.

 

Darey amesema alisukumwa kutoa wimbo huo ambao unaonyesha ukuu wa Mungu, ambaye ndiye pekee mwenye kuweza kutusaidia katika shida zetu za kila siku kupitia ukuu wake wa ajabu kutokana na magumu wanayopotia binadamu katika nyakati hizi.

 

Picha za video ya kibao hicho zilizochukuliwa jijini Lagos, Nigeria muongozaji akiwa ni Mex Ossai, zimepigwa kwa ustadi wa hali juu zikiangazia maisha halisi ya Kiafrika.

“Wimbo wangu mpya, “Jah Guide Me” unanirudisha kwenye kile ninachokipenda zaidi, ubunifu wa mashairi yake unagusa maisha ya kila mtu kwenye jamii ya sasa,” amesema Darey na kuongeza:

 

“Ni ujumbe uliokuja katika wakati mwafaka kwenye maisha ya sasa; wakati ambao binadamu tunapita kwenye changamoto ya haki za binadamu, lakini tukiwa na sala, shukrani na kumsifu Mungu kiroho zaidi, tukiamini nguvu itokayo juu, tutasalimika katika kipindi hiki kigumu.”

 

Darey ambaye ni mtoto wa mkongwe wa mwanamuziki wa African Jazz, Alade, anamiliki tuzo kadhaa za muziki kama Mwanamuziki Bora, Mwandishi Bora, na Mtayarishaji Bora.

 

Kutokana na ubora wake, Darey amewahi kupanda jukwaa moja na mastaa kadhaa wa ulimwenguni, wakiwemo Beyoncé, Wizkid, Jay Z, Ciara, Cardi B, Burna Boy, Sean Paul, Usher, R Kelly, Akon, Lionel Richie na wengine wengi.

 

Baadhi ya albamu zake mpaka sasa ni pamoja na From Me 2 U, unDAREYted na Double Dare, ambapo amekwishauza mamilioni ya albamu zinazozidi kumpaisha kwa mashabiki wa Afrika na nje ya bara hili.

 

STORI: JOSEPH SHALUWA

Leave a Comment