×

Kimenuka Barca! Mashabiki Wavamia Camp Nou ‘Messi Asiondoke’

 

KIMENUKA! Hivyo ndivyo unavyoweza kusema baada ya maelfu ya mashabiki ya Barcelona kuacha vitanda vyao usiku kuamkia na kuingia barabarani kuandamana wakielekea Nou Camp kuonyesha msisitizo wao wa kutofurahishwa na namna bodi ya klabu hiyo inavyoshughulikia suala la superstar wao, Lionel Messi ambaye anataka kusepa.

 

Messi ambaye ni raia wa Argentina amewasilisha maombi yake kwa uongozi wa Klabu ya Barcelona kutaka kuondoka baada ya kuitumikia klabu hiyo kwa muda mrefu na mafanikio makubwa lakini msimu huu mambo yakawa hovyo baada ya kumaliza nafasi ya pili kwenye La Liga huku wakiondolewa kwenye nusu fainali ya Champions League kwa kipigo cha bao 8-2 shidi ya Bayern.

 

Messi mwenye umri wa miaka 33 ambaye ni nahodha wa  Barca inaelezwa kuwa tayari ameshafanya mazungumzo na kocha mpya wa Barcelona, Ronald Koeman, juu ya azma yake ya kuondoka klabuni hapo ili akasake changamoto kwingine.

 

Wakati sakata la Messi likizidi kushika vichwa vya habari kuna taarifa za  kocha Ronald Koeman kuzidi kutofautiana na mchezaji Luis Suarez juu ya hatma yake katika kikosi cha Barcelona,  hali iliyozidi kuzua taharuki ndani ya klabu hiyo.

 

 

Suarez ambaye ni rafiki wa karibu na Messi, ni miongoni mwa wachezaji wanne ambao ni Rakitic, Vidal na Umtiti walioelezwa na kocha Koeman kupitia mawasiliano ya simu kuwa hawahitaji ndani ya klabu.

 

Inadaiwa huenda maamuzi ya kocha huyo wa zamani wa Everton kuhusu kutowataka Suarez na wenzake ni  sababu iliyochangia maamuzi ya Messi naye kuomba kuondoka Barcelona.

Leave a Comment