MABONDIA wa ngumi za kulipwa nchini, Abdallah Pazi ‘Dulla Mbabe’ na Twaha Kiduku wanatarajia kupambana leo Ijumaa katika pambano lao la ubingwa wa Taifa.
Mabondia hao watapanda ulingoni kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar baada ya jana kupima uzito kwenye Uwanja wa Kinesi tayari kwa pambano hilo lenye upinzani wa aina yake kutoka kwa mabondia wote wawili kuwahi kutoka sare katika pambano lao la nyuma.
Pambano hilo ni la uzito wa kati raundi 12, ambapo Dullah Mbabe ameliambia Championi Ijumaa kuwa safari hii mpinzani wake ameyakanyaga kwani hataweza kutoka kwenye mikono yake kutokana na alivyojipanga kurudisha heshima yake.
“Mdogo wangu Kiduku ameyakanyanga, sina huruma naye kwa sababu nimejipanga vizuri kuhakikisha hawezi kuchomoka hata iweje lazima nimkalishe ili kumfundisha adabu,” alisema Dullah Mbabe.
Kwa upande wa Kiduku alisema: “Binafsi kuongea siyo kazi yangu lazima ajue kwamba kesho (Ijumaa) si ndiyo tunakiwasha basi hataweza kutoka, hilo nawaambia mjue.”

