KOCHA msaidizi wa klabu ya soka ya Simba, Seleman Matola amewatahadharisha wapinzani wao msimu huu kwa kuwaambia wajipange sawasawa kwa kuwa Simba inataka tena kutetea mataji yake yote.
Akizungumza na Championi Jumatano, Matola ambaye kuanzia amejiunga na Simba katikati ya msimu uliopita amechukua mataji matatu, FA, Ligi Kuu Bara na Ngao ya Jamii, alisema kuwa wanakwenda Mbeya kwa tahadhari kubwa.
“Timu yetu inaendelea vizuri na maandalizi ya msimu mpya wa 2020/21, ambapo mchezo wetu wa kwanza utakuwa dhidi ya klabu ya soka ya Ihefu Jumapili, tunaiheshimu Ihefu licha ya ugeni wao kwenye Ligi Kuu Bara kwani tunaamini kila timu imejiandaa vizuri kushindana.
“Kwa kutambua hilo tumeiandaa timu yetu katika mazingira ya kuhakikisha inakusanya pointi tatu muhimu kwenye kila mchezo kwa kuwa tunaamini kuwa mchezo wowote ulio mbele yetu ni fainali hivyo ni lazima tupambane kupata matokeo mazuri,” alisema Matola.
Simba jana ilisafiri kwa ndege kutokea Jijini Arusha kuelekea Mbeya kwa ajili ya maandalizi ya mwisho ya mchezo huo wa ufunguzi wa ligi dhidi ya Ihefu unaotarajiwa kupigwa Septemba sita.
Stori: Joel Thomas, Dar es Salaam


