MTENDAJI Mkuu wa Bodi ya Ligi Kuu nchini Tanzania (TPLB), Almasi Kasongo, amewataka wamiliki wa viwanja vinavyochezewa Ligi Kuu soka nchini Tanzania (VPL) wajiandae na rungu kutoka bodi hiyo.
Akiongea na Kipenga hii leo mtendaji huyo amesema kuwa kwa viwanja vyovyote ambavyo vitakiuka sheria namba moja ya Sheria ya Mpira wa Miguu Ulimwenguni ya FIFA inayozungumzia uwanja kwa ajili ya mchezo wa mpira wa miguu.
“Jambo zuri ambalo ninafurahia ni kuwa sisi sote kwa pamoja wetu tunaridhika kwamba hivi viwanja vilivyofungiwa kweli havikidhi viwango, havikidhi matakwa ya kikanuni ya sheria namba moja katika sheria namba 17 ya mpira wa miguu,” amesema.
Itakumbukwa kuwa hadi sasa tayari viwanja viwili vimeshafungiwa kwa kutokidhi vigezo tangu kuanza kwa msimu mpya wa VPL 2020-21 Septemba 6, mwaka huu. Viwanja hivyo ni pamoja na uwanja wa timu ya Gwambina uliopo Misungwi mkoani Mwanza na uwanja wa Musoma unaotumiwa na Biashara United.
Aidha, amekiri kuwa upya wa mfumo wa kielektroniki katika kuingia viwanjani ndiyo chanzo cha changamoto iliyojitokeza siku ya jana Uwanja wa Mkapa katika mechi iliyowakutanisha Yanga na Mbeya City.
“Kama unavyojua, mzabuni ni mpya na inawezekana hana uzoefu huo, ila kadri mechi zinavyoendelea naamini watakuwa bora, lakini pia watazamaji wajitahidi kuingia mapema viwanjani,” amesema.
