×

Anaswa na Kichwa cha Mtoto Mbele ya Bunge

POLISI nchini Uganda wametibitisha kuwa kichwa cha mtoto kilichokatwa, kilichopatikana katika kikapu cha mwanamme aliyekamatwa kwenye lango la bunge nchini Uganda Jumatatu, kilikuwa ni sehemu ya mwili uliopatikana katika wilaya ya Masaka, kusini-magharibi mwa mji mkuu Kampala.

 

Idara ya upelelezi wa makosa ya jinai nchini humo imesema wachunguzi watafanya kipimo cha vinasaba (DNA) kwa wajumbe wa familia moja ya Masaka ambao waliripoti kupotea kwa mtoto wao, kubaini iwapo kweli mtoto huyo aliyekatwa kichwa ni wao.

 

Familia iliyompoteza mtoto iliviambia vyombo vya habari nchini humo Jumanne, kwamba walikuwa wamemuajiri Joseph Nuwashaba, mwenye umri wa miaka 22, ambaye alipatikana na kichwa cha mtoto, kama mfanyakazi wa shamba lao.

 

Uchunguzi bado unaendelea kubaini ni yapi yalikuwa malengo ya  Nuwashaba, na polisi wamesema watafanya uchunguzi  wa akili yake.

 

Alipokamatwa, Nuwashaba aliwaambia maafisa katika bunge kwamba alitaka kuwasilisha mzigo uliokuwa na kichwa kwa Spika wa Bunge, Bi Rebecca Kadaga. Spika hajatoa kauli yoyote juu yatukio hilo, na aliwaambia wabunge kuwa anasubiri matokeo ya uchunguzi wa polisi.

Leave a Comment