
Bodi ya Korosho nchini kwa kushirikiana na taasisi mbalimbali ikiwemo TMX, WHI na nyinginezo kutoka ndani na nje ya nchi leo wamefanya warsha na wadau kujadili jinsi ya kuinua zao hilo hapa nchini. Warsha hiyo imefanyika Jengo la LAPF Milleniun Tower Jijini Dar
Akizungumza kwenye warsha hiyo, Mwenyekiti wa Chama cha Wabanguaji Wakubwa nchini, Bahati Mayoma amesema warsha hiyo imelenga kuinua sekta ya korosho ambayo imekuwa na changamoto kwa muda mrefu.

Mayoma amesema kwa zaidi ya miaka kumi ubanguaji umekuwa chini ya asilimia kumi.
“Hii imepelekea ajira nyingi zilizokuwa zikipatikana kwa kazi ya ubanguaji korosho kupotea.

Korosho ghafi zimekuwa zikipelekwa nje ya nchi ambapo huko wakishazibangua na kuziboresha wanaziweka nembo za nchi zao na kuziuza kwa bei kubwa zaidi”. Alisema Mayoma.
Mayoma aliendelea kusema kuwa malengo ya warsha hiyo waliyowashirikisha wadau kutoka nchi za nje ni kuhakikisha wanabadilishana uzoefu katika uboreshaji wa zao hilo ambalo linazalishwa kwa wingi hapa nchini.

Alimalizia kwa kusema malengo ya warsha hiyo kufikia mwaka 2024 mpaka 2025 nusu ya korosho inayopelekwa nje ya nchi iwe inabanguliwa hapa nchini.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Tanzania Private Sector Foundation, Zachy Mbenna amesema zao hilo hapa nchini linakadiriwa kuwa na thamani ya zaidi ya bilioni 250 za Kimarekani na kuwataka wadau kuamka nalo ambapo linaonekana kama limesakusahaulika.

“Hili zao tukiwa nalo makini litawainua wadau kama Tanzanite yetu ilivyomuinua mchimbaji mdogo hapa nchini baada ya kuipa umuhimu sekta ya madini kufikia hatua ya kuuzunguushia ukutani mgodi wa madini hayo”. Alisema Mbenna.
Wengine waliochangia mada mbalimbali kwenye warsha hiyo ni pamoja na Mhadhiri kutoka Chuo cha Mwalimu Nyerere Academy Dkt. Geni Kasoga, Mkurugenzi wa Soko la Bidhaa nchini, Agustino Mburumi na wengineo.
