RAIS wa Tanzania na mgombea urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), John Magufuli, ametuma salamu za pole na ubani wa shilingi milioni tano kwa familia, kufuatia mauaji na kifo cha aliyekuwa Mwenyekiti wa Wanafunzi wa Vyuo na Vyuo Vikuu (UVCCM) mkoa wa Iringa, Emmanuel Mlelwa, aliyeuawa hivi karibuni na watu wanaodaiwa kuwa ni wa vyama vya upinzani.
Akizungumza wakati wa kutoa salam za rambirambi Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM (NEC) Uchumi na Fedha wa CCM ambaye pia ni mlezi wa chama hicho Mkoa wa Njombe, Frank Hawasi, kwa niaba ya Dkt. Magufuli amesema, “Rais Magufuli na Mwenyekiti wa CCM amepokea taarifa ya kifo cha kijana wetu Emmanuel Mlelwa kwa masikitiko makubwa sana, kwa sababu sio kifo cha kawaida.”
Rais magufuli ameviagiza vyombo vyote ulinzi na usalama kuhakikisha wanafuatilia jambo hili na kuwakamata wahusika wote bila kujali vyama na kuwafikisha mahakamani ili sheria ichukue mkondo wake.
Aidha, Mkuu wa mkoa wa Njombe, Mhandisi Marwa Rubirya, amesema kuwa tayari watuhumiwa wawili, wanashikiliwa na polisi kufutia kifo hicho cha kikatili kilichotokea Septemba 20 na mwili wake kutupwa na watu wasiojulikana.
Rubirya, ametoa kauli hiyo wakati wa mazishi ya Mlelwa, yaliyofanyika katika kijiji cha Luvuyo kilichopo Kata ya Madope wilayani Ludewa.
Kwa upande wake, RPC Njombe, Hamis Issah, amesema; “Hili tukio kweli limetokea na polisi tunayo taarifa, ingawa lilikuwa linaonekana kwenye mitandao lakini sasa limefikia mahali pake.
“Sasa mimi nitawaleteeni kitu ambacho ni sawa sawa, nani amekamatwa na nani anahusika vipi na kila kitu ambacho kinaendelea kuhusu tukio hili nitatoa taarifa rasmi kupitia vyombo mbalimbali vya habari,” alisema ACP Issah.
Mlelwa aliyekuwa mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Iringa alikuwa mkoani Njombe kwa ajili ya likizo na alitoweka tangu Septemba 20.


