UONGOZI wa Yanga umeibuka na kusema kuwa kiungo wao mshambuliaji, Farid Mussa haonekani katika kikosi cha timu hiyo baada ya kupewa ruhusa maalum kutoka kwa mabosi wake.
Farid ni kati ya wachezaji wapya waliojiunga na Yanga katika msimu huu wa ligi akitokea Tenerife ya nchini Hispania kama mchezaji huru baada ya kumalizana na waajiri wake.
Kiungo huyo hakuwepo kwenye msafara wa timu hiyo uliokwenda Morogoro kucheza na Mtibwa Sugar katika mchezo wa Ligi Kuu Bara uliopigwa Uwanja wa Jamhuri mkoani humo wikiendi iliyopita.
Akizungumza na Championi Jumatano, Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Frederick Mwakalebela, alisema kuwa kiungo huyo haonekani kikosini kwa kuwa alipewa ruhusu akajitibu.
Mwakalebela alisema kuwa, Farid hana tatizo lolote na benchi la ufundi na sasa yupo na timu kambini kwenye kijiji cha Avic Town kilichopo Kimbiji, Kigamboni akijiandaa na mchezo wa ligi dhidi ya Coastal Union utakaopigwa Uwanja wa Mkapa, Dar.
“Farid alipewa ruhusu maalum baada ya kuugua Malaria, hata hivyo sasa hivi anaendelea vizuri. Mashabiki wasiwe na wasiwasi siku siyo nyingi mtamuona kijana wenu uwanjani.
“Kwani mashabiki wanafahamu uwezo wa Farid na kikubwa wanatamani kumuona akiwepo uwanjani akiipambania timu yake ya Yanga katika msimu huu na tayari amesharudi kambini,” alisema Mwakalebela.
