ALIYEWAHI kuwa Mwenyekiti wa Klabu ya Simba, Ismail Aden Rage amemtaka Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Fredrick Mwakalebela aache kuwadanganya mashabiki wa timu hiyo kuhusiana na ishu ya mkataba wa kiungo mshambuliaji wa Simba, Bernard Morrison.
Juzi Klabu ya Yanga kupitia Mwakalebela ilitoa malalamiko ya kupinga mkataba wa Morrison aliosaini kuichezea Simba kwa kuwa siyo halali kutokana na upungufu ambao aliubainisha mbele ya Waandishi wa Habari.
Aidha, katika hatua nyingine Yanga inadai kulipeleka shitaka la Morrison Mahakama ya Usuluhishi wa Michezo ‘CAS’ ili kuweza kupatiwa ufumbuzi zaidi baada ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kupitia Kamati ya Maadili kulitupilia mbali jambo hilo.
Rage aliliambia Championi Jumamosi kuwa, iwapo mkataba wa Simba na Morrison utakuwa na upungufu wanaotakiwa kulalamika ni pande hizo mbili walioingia mkataba na kudai kuwa iwapo Simba wakiamua wanaweza kumfungulia mashitaka.Aliongeza kuwa, ameshangaa na kusikitika kuona madai yanayotolewa na Yanga chini ya Mwakalebela ambaye aliwahi kuwa katibu TFF kwa kuwapotosha Wanayanga juu ya suala la Morrison huku akijua wazi ukweli ulivyo.
“Nimeshangaa na kusikitika madai haya yametolewa na Yanga chini ya Mwakalebela ambaye alikuwa kiongozi wa TFF aweke wazi kila kitu, kisheria mkataba wa watu wawili hauwezi kuingiliwa na mtu mwingine kati kama una mapungufu ya aina yeyote wanaotakiwa kulalamika ni Simba ama mchezaji mwenyewe Morrison.“Simba wanaweza kuwashitaki, yeye amepataje nyaraka za mkataba ambao ni siri ya watu wawili.
“Sheria za Caf na Fifa kuna muda wa vipingamizi je kipindi hicho mbona walikaa kimya, kuna kipengele cha mkataba kinasema kuwa ‘voidable contract’ ni mkataba uliokamili, kama kuna mapungufu yule mmoja wapo anatakiwa alalamike.
“Hivyo, kinachotakiwa wao wenyewe wakubaliane kuurekebisha na inaruhusiwa na mchezaji anaendelea kuitumikia timu yake na iwapo hakutakuwa na makubaliano baina ya pande hizo mbili basi mkataba unaweza kuvunjika,” alisema Rage.
Aidha, kwa upande wake, Mshauri wa Mwenyekiti wa Bodi ya Klabu ya Simba, Crescentius Magori yeye alisema: “Yanga wao wameupata wapi mkataba wa Morrison na Simba? Mkataba wa Morrison na Simba, TFF na FIFA ndiyo wanaweza kuuona Yanga wao wameupata wapi?
Alihoji na kuongeza:“Nauliza wameupata wapi? Wanahangaika na mkataba wa Morrison ili iweje, wao walishashindwa kesi na Morrison, wanashindwa kuhangaika na masuala ya maana wanahangaika na mkataba wa Morrison, aibu sana.
“Wanachotakiwa kuiandaa timu yao ili ipate matokeo mazuri katika michezo inayofuatia ya ligi lakini siyo kuwa bize na suala hilo ambalo tayari limefungwa na shirikisho baada ya kushindwa kesi yao.
“Sisi kwa upande wetu Simba, hatutaki kulizungumzia hilo suala ambalo tayari muafaka wake umemalizika kwa TFF kuridhia Morrison kujiunga na Simba.”
STORI: Khadija Mngwai na Wilbert Moland

