MSHAMBULIAJI wa Yanga, Mghana, Michael Sarpong amekiri kuwa amekuwa akipata wakati mgumu katika kila mchezo wa ligi kuu kutokana kukamiwa na mabeki wa timu pinzani lakini amesisitiza hali hiyo haimtishi kuendelea kuipambania timu yake.
Sarpong amejiunga na Yanga kwa mkataba wa miaka miwili akitokea Rayon Sport ya nchini Rwanda ambapo mpaka sasa amefanikiwa kucheza mechi za ligi kuu msimu huu lakini akiwa amefunga bao moja pekee.
Akizungumza na Championi Jumamosi, Sarpong alisema kuwa, amekuwa akikutana na wakati mgumu kutoka kwa mabeki wa timu mpinzani kutokana na kucheza kwa kumkamia lakini kwake jambo hili haliwezi kufanya akate tamaa kwani anajua vizuri kazi yake.
“Suala la ugumu wa ligi, kweli ni ngumu lakini changamoto kubwa ambayo naona kwa sasa ni mabeki wa timu pinzani kucheza kwa kukamia yaani mtu anakuja kwa ajili ya kucheza kwa kukomoa ili ushindwe.
“Lakini kwa upande wangu siwezi kutishika kwa wao namna wanavyopambana kunizua kwa sababu kitu cha msingi ambacho nakiangalia ni kuona timu inapata matokeo katika kila mchezo haijalishi kama nimefunga mimi au vipi,” alisema Sarpong.
Ibrahim Mussa, Dares Salaam
