×

Yanga Yaibua 440m za Morrison

SHIRIKISHO la Soka la Tanzania (TFF) kwa sasa ndilo pekee ambalo linasubiriwa kutoa majibu kuhusu utata wa mkataba wa mshambuliaji wa Simba, Bernard Morrison baada ya Yanga kuibua tuhuma kadhaa kuhusu mkataba wa mchezaji huyo na muajiri wake.

 

Yanga imeibua taarifa kuwa kuna tatizo la kimkataba ambapo wiki jana waliibuka na mkataba wanaodai kuwa ni wa Morrison na Simba na kufunguka kuwa haujasainiwa na pande mbili pamoja na watu wengine kadhaa, ambapo wameitaka TFF kuupitia na kuishawishi kuwa Simba hawana uhalali wa kummiliki mchezaji huyo.

 

Achana na ishu hiyo ya kutosainiwa na CEO, mjumbe wa Bodi ya Simba au mwanasheria au shahidi wa Morrison, Championi Jumamosi limeuchunguza vizuri mkataba huo uliosambazwa na Yanga ambao wanasema wameupata katika mfumo wa usajili wa TMS na kubaini mambo kadhaa ya muhimu.

 

MSHAHARA WA MORRISON

Mkataba huo ambao unaanza rasmi kutumika Agosti 14, 2020 na kuendelea kwa muda wa miaka miwili inaonyesha kuwa mshahara wa Morrison kwa mwezi ni dola 5,500.Kiwango hicho ni sawa na Sh milioni 12.6 kwa mwezi, ikiwa na maana kuwa kwa muda wa miezi 12 ambayo atakuwa muajiriwa wa Simba ataingiza jumla ya Sh 302.4 kama malipo ya mshahara.

 

DAU LA USAJILI

Mkataba huo unaonyesha kuwa Simba ilikubali kulipa dola 60,000 (Sh 138.4) kwa ajili ya malipo ya usajili, akiwa ni mchezaji huru, kiwango ambacho alikipokea mchezaji mwenyewe kwa sababu tayari alikuwa ameshaachana na Yanga.

Ukijumlisha kiwango cha malipo ya mshahara na dau la usajili alilolipwa mchezaji inamaanisha kuwa jumla Morrison ataingiza Sh 440.8 kwa muda wa miaka miwili, hapo ni mbali na posho na malipo mengine ambayo atakuwa anayapata.

 

ANAUZWA SH BILIONI 1.3

Mkataba huo ambao Yanga wamedai kuwa ni halali unaonyesha kuwa ikiwa kuna klabu inataka kumsajili kabla ya kumaliza mkataba wake, basi italazimika kulipa dola 600,000 (Sh bilioni 1.3) kwa Simba.

 

MORRISON HANA WAKALA?

Katika moja ya kipengele cha mkataba huo kinaonyesha kuwa kama Morrison akiuzwa wakati wa mkataba wake, basi yeye na wakala wake watalipwa asilimia 10 ya malipo hayo ya usajili.Lakini kipengele hicho ambacho kinaonyesha jina la wakala linatakiwa kuwekwa, hakuna jina lolote, pako wazi lakini Yanga hawajazungumza chochote kuhusu kipengele hicho.

 

Hoja hiyo inaweza kukolezwa na uhalisia kuwa mara kadhaa katika mashauri ya kesi yake dhidi ya Yanga iliyotikisa hivi karibuni, Morrison hakuonekana kuwa na wakala, alikuwa akisimama mwenyewe kwenye shauri lake wala hakuna aliyewahi kujitokeza kuzungumza kuwa ni wakala wa Mghana huyo.

 

 Alhamisi iliyopita, Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Fredrick Mwakalebela ndiye ambaye alizungumza na waandishi wa habari na kufafanua suala hilo la mkataba ambapo TFF wamekiri kupokea na wanalifanyia kazi.

John Joseph, Dar es Salaam

Leave a Comment