MGOMBEA ubunge Jimbo la Buchosa kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Eric Shigongo James, amesema iwapo atachaguliwa hatakubali wananchi wa Jimbo lake linalozungukwa na Ziwa Victoria kuona miradi ya maji inayotoka katika maeneo hayo inapita na kwenda maeneo mengine ya mbali wakati wao wakikosa maji safi na salama.
Amesema hayo wakati akifanya mkutano wake wa kampeni jana Jumatatu, Oktoba 5, 2020 na wananchi katika Kijiji cha Nyakaliro kuwaomba ridhaa ya kuwa mwakilishi wao bungeni kwa miaka mitano ijayo.
“Kama hii ni Ilani ya CCM na imetaja hivyo, kwa nini maji yapite hapa kwenye ardhi yetu na ziwa lile pale, yaende huko na watu wa hapa wakose maji, mama zangu wahangaike na ndoo kwenda kutafuta maji mbali, nani atakubali? Haiwezekani, Mimi sitakubali, hilo niachieni mimi, mtaona nitavyofanya, nitagombana nao na maji yatakuja hapa,
“Matatizo tunayo mengi, barabara, elimu, zahanati na mengine mengi, hayo niachieni mimi nitashughulika nayo, uwezo ninao, nia ninayo na moyo ninao, ninataka nifanye mambo ambayo hata siku moja nisipokuwa hapa duniani watu waseme alikuwepo mtu aliishi aliitwa Shigongo, alifanya hiki na hiki.
“Nimesema nitanunua katapila langu mwenyewe kwa pesa zangu, kwa ajili ya kutengeneza barabara, nchi hii ni kubwa si kila jambo serikali itafanya, mambo mengine tutafanya wenyewe, katapila lile tutaweka mafuta litachonga barabara zetu, nashindwaje kununua greda langu? Sio la halmashauri, la kwangu, wewe weka mafuta chonga barabara.
“Vijana nataka mnielewe, tuchape kazi, hatuwezi kuwa na shule haina choo, watoto wetu wanajisaidia vichakani, hapana, hatuwezi kusubiri serikali ije ituchimbie shimo la choo, tutafanya wenyewe, nataka baada ya miaka mitano au kumi tuseme Buchosa ni bora kuliko wakati uliopita,” aliahidi kwa msisitizo Shgiongo .
Mgombea huyo anaendelea na kampeni zake jimboni Buchosa akinadi sera za chama chake cha CCM pamoja kuwaomba ridhaa wananchi ili wawachague viongozi wa CCM kuanzia kiti cha urais, ubunge na udiwani katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 28, mwaka huu.
