×

TFS na Unesco Wasaini Mkataba Kuboresha na Kulinda Michoro ya Miambani Kondoa

Dar es Salaam: Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania – TFS chini ya Wizara ya Maliasiili na Utalii, imesaini Mkataba wa Utekelezaji wa Mradi wa Michoro ya Miambani Kondoa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) ili kuhakikisha maeneo hayo yenye umuhimu mkubwa wa kitamaduni kwa binadamu yanalindwa na kuhifadhiwa.

Akizungumza katika hafla ya utiaji saini Mkataba huo iliyofanyika Jijini Dar es Salaam leo Octoba 6, 2020, Katibu Mtendaji wa Tume ya Taifa ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (NATCOM-Unesco), Profesa Hamisi Malebo alisema mkataba huo wa mwaka mmoja wenye thamani ya dora za Kimarekani 30,000 utakwenda kuboresha na kuimarisha urithi wa nchi.

 

“Nafurahi kuona leo wenzetu wa TFS wanatiliana saini mkataba unaokwenda kuboresha na kuimarisha urithi wetu, Tume imeshiriki mchakato mzima wa uombaji wa fedha hizi na niseme wazi, kupitia mkataba huu sasa michoro ya Miambani Kondoa inakwenda kusafishwa, kuwekewa ulinzi utakaohakikisha eneo hilo linabaki salama,”

“Lakini pia mkataba huu unaenda kuifanya michoro iliyopo isipatwe na changamoto yoyote yakuifanya ipotee lakini pia kulifanya eneo hilo kuwa sehemu salama ya kufanyia shughuli za utalii,” alisema Prof. Malebo.

 

Kwa upande wake Kamishna wa Uhifadhi – TFS Prof. Dos Santos Silayo, alisema Mwaka 2006 eneo la michoro ya Kondoa Irangi liliingizwa katika orodha ya Urithi wa dunia na kuandaliwa mpango wa usimamizi wa miaka 10 ambao umemalizika miaka 4 iliyopita na sasa wanatekeleza mradi mwingine wa kuhuhisha mpango wa usimamizi wa eneo hilo.

“Sasa tunatekeleza mradi uliodhaminiwa na Unesco kwa dora za Kimarekani 30,000, utekelezaji wa mpango huu ni mkakati wa TFS kuhakikisha kwamba maeneo ya urithi wa dunia na mambo ya kale yanaendelezwa ili kuhakikisha kwamba yanatoa mchango mkubwa katika sekta ya elimu, utamaduni na hata kuweza kuyatumia maeneo hayo kuzalisha fedha kwa ajili ya utunzaji wa maeneo hayo pamoja na maendeleo ya taifa,”

 

“katika mipango tunayokwenda kutekelezwa katika kipindi cha mwaka huu mmoja, ni kuhakikisha maeno haya yanakuwa salama, kuishirikisha jamii inayozunguka michoro hii kutambua umuhimu wa maeneo yao katika urithi wa dunia, lakini zaidi ni urithi wao kwa sababu kiutamaduni wao ndio wameishi katika maeneo haya na mambo yaliotokea humo jamii inastahili kuyaenzi kwa faida yao lakini dunia kwa ujumla wake” alisema Prof. Silayo.

Naye Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Malikale, Dkt. Fabian Kigadye, alisema tukio hilo ni fursa nzuri kwa idara yake kuona taasisi zilizokasimiwa kusimamia vituo vya Michoro ya Kondoa, magofu ya Kilwa Kisiwani na Songo Mnara zinachukua juhudi za kuviendeleza na kuviboresha vituo hivyo ili view vivutio vikubwa vya utalii nchini.

 

Wakati huo huo Unesco imemesaini mkataba wa dora za Kimarekani zaidi ya 28,000 na Mamlaka ya Wanyamapori Tanzania – TAWA kwa ajili ya kuhakikisha magofu ya Kilwa Kisiwani na Songo Mnara yanapandwa mikoko itakayokwenda kuzuia mawimbi ya bahari kubomoa magofu hayo.

Tirso Dos Santos ni Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la elimu, sayansi na utamaduni, UNESCO jijini Dar es Salaam anasema taasisi zote zilizopata fedha azihakikisha zinatumia ndani ya muda na kwa malengo ya mradi na si vinginevyo.

Michoro ya Kondoa inayopatikana wilayani Kondoa mkoani Dodoma nchini inatazamwa kutoa ushuhuda wa namna ya maisha ya wachoraji waliokuwa wawindaji kutokana na kuonyesha picha za watu, wanyama na uwindaji.

Leave a Comment