Kumekucha! Hivyo ndivyo unavyoweza kusema kufuatia kufungwa na kuwashwa rasmi kwa satelite ya kituo kikubwa cha matangazo ulimwenguni, Voice of America ya nchini Marekani (kwa Trump) katika ofisi za Global Group zilizopo Sinza Mori jijini Dar es Salaam.
Kuwashwa kwa satelite hiyo, sasa kutawawezesha watazamaji na wasikilizaji wa Global TV na Global Radio, kuyapata matangazo ya moja kwa moja kutoka Voice of America inayotangaza kutoka jijini Washington, Marekani kupitia simu zao kwa urahisi zaidi.
Huu ni mwendelezo wa ushirikiano wa nguvu kati ya Voice of America na Global TV na +255 Global Radio, wa kuhakikisha mtazamaji na msikilizaji, hapitwi na jambo lolote linaloendelea ulimwenguni kupitia simu yake.
Akizungumza katika Kipindi cha Front Page kinachorushwa kupitia Global TV na +255 Global Radio, Meneja wa Global Group, Abdallah Mrisho, amesema lengo la ushirikiano huo ni kuongeza wigo kwa Watanzania kupata taarifa kwa undani zaidi kwenye nyanja zote na kujua kila kinachoendelea duniani.
“Tumewasha mtambo kutoka Voice of America, ambapo sasa tunao uwezo wa kupata matangazo ya moja kwa moja kutoka kituo hicho kikubwa duniani kinachofadhiliwa na Serikali ya Marekani.
“Kwa ambao hawajui, Voice of America inatangaza matangazo yake kwa zaidi ya lugha 47 duniani, ikiwemo Kiswahili, ikiwa imedumu kwenye tasnia ya matangazo ya redio na runinga kwa zaidi ya miaka 78.
“Kwetu sisi ni fahari kubwa sana lakini pia ni fahari kwa wasikilizaji na watazamaji wetu, kama bado huja-subscribe Global TV na kudownload app ya Global Radio, wahi ili usipitwe kwa sababu kazi ndiyo kwanza imeanza, mengi makubwa yanakuja.
“Tayari tumeanza kurusha vipindi kama Duniani Leo kinachohusu habari mchanganyiko zilizotokea duniani kote, kila siku saa tatu kamili kupitia Global TV, ambapo utakutana na watangazaji mahiri na wakongwe kama Mary Mgawe, Idd Ligongo, Mkamiti Kibayasi, Keneth Bwire na wengine wengi ambapo sasa utakuwa unawaona kila siku wakitangaza kwa lugha ya Kiswahili.
“Lakini pia kuna kipindi cha Kiingereza cha kuchambua mambo mazito na kuwahoji watu wazito duniani cha Straight Talk Africa kinachoongozwa na mtangazaji mkongwe, Tshaka Ssali.
“Hiki pia tayari kinaonekana kupitia Global TV kila siku ya Alhamisi, saa tatu kamili asubuhi, kikiongozwa na mtangazaji mkongwe, Shaka Ssali, pamoja na kipindi kingine cha Washington Bureau kinachorushwa na mtangazaji Mtanzania, Sunday Shomari.
“Kuna kipindi kingine cha Zulia Jekundu ambacho kina-cover habari zote za burudani za wasanii wa kimataifa kutoka sehemu mbalimbali duniani, kikitangazwa na mtangazaji Harrison Kamau kila siku ya Jumamosi, saa saba kamili mchana kupitia Global TV.
“Kipindi kingine kipya tunachokwenda kukiongeza kwenye orodha yetu, ni Maisha na Afya ambacho ni mahsusi kwa ajili ya kuchambua kwa kina jinsi ya kujikinga na magonjwa mbalimbali pamoja na mfumo mzuri wa maisha, kikitangazwa kwa Lugha ya Kiswahili na kitakuwa kikiruka kupitia Global TV kila Jumamosi saa saba na robo mchana.
Mrisho ameendelea kueleza kuwa kwa upande wa redio, +255 Global Radio, tayari inaungana na VOA kila siku saa 12 asubuhi katika kipindi cha Kumekucha Afrika ambapo unapata habari zote ‘latest’ zilizojiri Afrika na Marekani, huku kipindi kingine cha Kwa Undani kikitarajiwa kuanza kuruka kuanzia Jumatatu hadi Alhamisi, saa tatu mpaka saa tatu na nusu usiku.
Pia kutakuwa na kipindi cha burudani ya muziki cha Top 20 Countdown kila Ijumaa ambapo utapata nafasi ya kusikiliza nyimbo bora zinazotamba duniani kote.
“Huu ni mwanzo tu, kuna mengi zaidi yanakuja, vipindi vitaongezeka zaidi kwa hiyo niwasihi wadau wote wa Global Radio na Global TV kukaa mkao wa kula, lakini pia nawashukuru Voice of America chini ya kiongozi wao, Mwamoyo Hamza kwa kushirikiana nasi kuhakikisha habari zinawafikia watu wengi zaidi kwa urahisi kupitia ‘platforms’ zetu zenye nguvu zaidi Tanzania,” anahitimisha Mrisho.
Na Mwandishi Wetu,


